BUJUMBURA : Kundi la waasi Burundi lamkataa kiongozi wao
10 Oktoba 2005Kundi la waasi wa Burundi limesema leo hii wanamkataa kiongozi wao na kumshutumu kwa ukiukaji mkubwa wa haki za binaadamu ikiwa ni kama shinikizo kwa kundi la mwisho la waasi lililobakia katika taifa hilo kuingia kwenye mazungumzo ya amani.
Msemaji wa kundi hilo lenye wanachama 260 wa Kihutu wa FNL wamesema uamuzi wao wa kuvunja uhusiano na kiongozi wa waasi Agathon Rwasa umefikiwa mwishoni mwa juma na wanamshutumu kiongozi huyo kwa kuuwa watu wasiokuwa na hatia na kwa kuwakata vichwa watu anaowatuhumu kuwa na ushirikiano na jeshi.
Kundi hilo hilo limesema mwezi uliopita kwamba limechoshwa na vita na kumtaka Rwasa akubali pendekezo la muasi aliyegeuka kuwa Rais Pierre Nkurunziza la kutaka mazungumzo ya amani.
Haijulikani iwapo wapiganaji wa FNL wanaunga mkono hatua hiyo au la.
Msemaji wa kundi hilo Sylvestre Niyungeko amesema pia imewakataa viongozi wengine waandamizi wa FNL akiwemo kamanda wa kikosi Ibrahim Ntakarutimana na katibu mkuu Jonas Nshimirimana.