BUJUMBURA. Rais mpya wa Burundi aapishwa
26 Agosti 2005Rais mpya wa Burundi ameapishwa hii leo katika sherehe iliyofana mjini Bujumbura.
Kiongozi wa kundi kubwa la waasi wa zamani wa kabila la Hutu Pierre Nkurunziza ndie rais wa kwanza wa Burundi kuchaguliwa katika misingi ya kidemokrasia tangu nchi hiyo kutumbukia katika vita mwaka 1993.
Kuchaguliwa bwana Nkurunziza kuliongoza taifa la Burundi kumefikisha kikomo cha makubaliano ya miaka mitano ya serikali ya mpito yaliyoafikiwa ili kuleta maridhiano baina ya waliokuwa waasi wa Kihutu na utawala wa zamani wa kijeshi wa Watutsi.
Rais Pierre Nkurunziza ameahidi kugawa nafasi za kisiasa na kazi za kiserikali kwa jamii ya Burundi moja bila kuzingatia maswala ya kikabila ili kufanikisha makubaliano ya amani.
Safari ndefu ya kisiasa aliyoifanya rais Nkrunziza ni kaunzia kwenye ngazi ya ualimu, mpaka kiongozi wa kundi la waasi hadi leo hii ameapishwa kuwa rais wa Burundi.
Sherehe hiyo ya kuapishwa rais wa Burundi ilihudhuriwa na viongozi mbali mbali wa bara la Afrika.