1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Burundi yaanza mlolongo wa chaguzi

Sekione Kitojo20 Mei 2010

Taifa la Burundi leo linaanza mlolongo mrefu wa uchaguzi ambamo mahasimu wa zamani wanahitaji kuthibitisha kuwa wanaweza kushindana bila kuhatarisha makubaliano tete ya amani.

https://p.dw.com/p/NSoK
Vyama vya akina mama pia vinashiriki katika kuwahamasisha wanawake kupiga kura katika uchaguzi nchini Burundi.Picha: DW

Taifa dogo la Afrika ya kati la Burundi leo linaanza mlolongo mrefu wa uchaguzi ambamo mahasimu wa zamani katika vita vya wenyewe kwa wenyewe watahitaji kuthibitisha kuwa wanaweza kushindana bila ya kuathiri makubaliano tete ya amani yaliyofikiwa.

Kiasi cha wapiga kura milioni 3.5 wataingia katika vituo vya kupigia kura leo Ijumaa kuwachagua madiwani katika kile wachunguzi wa mambo wanasema ni mtihani mkubwa kwa wagombea wakuu katika uchaguzi mkuu ujao wa bunge pamoja na rais. Rais Pierre Nkurunziza na kiongozi wa zamani wa waasi Agathon Rwasa walifanya kampeni za hali ya juu kama za urais katika uchaguzi huo wa madiwani , wakizunguka huku na huko katika nchi hiyo.

Rais huyo mwenye umri wa miaka 45, mlokole alifanya kila juhudi hadi dakika za mwisho katika kampeni hiyo, siku ya Jumatano akihutubia makundi ya watu kwa nyimbo na kucheza.

Fanyeni kazi na kusali, alisema akiwa katika gari lake la kampeni , akiwa amevalia viatu vya kisasa vya raba, fulana na kofia ikiwa na maandishi ya nembo ya chama tawala cha CNDD-FDD.

Tutashinda uchaguzi huu. Ikiwa bado mnanihitaji , katika mwaka 2015 na 2020 , lakini iwapo mtapata mtu ambaye ni bora zaidi kuliko mimi, basi mpigieni kura na nitaondoka, amewaambia wafuasi wake mjini Bujumbura kuhusiana na uchaguzi wa rais wa hapo Juni 28. Uchaguzi wa bunge utafanyika mwezi Julai.

Wakati rais huyo kijana anapata manufaa kutokana na kuwa rais kwa sasa , ushindani ni mkali miongoni mwa vyama kutoka jamii ya Wahutu, ambalo ni kundi kubwa linalofikia kiasi cha asilimia 85 ya jumla ya watu wote nchini Burundi wanaofikia kiasi cha wakaazi milioni 8.5.

Uchaguzi uliomwingiza Nkurunziza madarakani mwaka 2005 ulionekana kwa kiasi kikubwa kuwa huru na wa haki, lakini changuzi kadha zinazoanza leo zitakuwa za kwanza ambapo vyama vyote vya nchi hiyo vinawakilishwa.

Kundi la mwisho la waasi wa Kihutu la National Liberation Forces, FNL , liliweka silaha chini mwaka jana na kuwa chama cha siasa likiongozwa na Agathon Rwasa.

Kampeni ya kiongozi huyo wa zamani wa waasi ilikuwa yenye uhai, lakini pia ya utulivu zaidi , ikilenga kukosoa matokeo ya utawala wa miaka mitano ya Nkurunziza.

Jibu la FNL kwa nembo ya chama tawala ya mfalme tai ni mtumbwi unaondeshwa na Rwasa binafsi akiipeleka Burundi katika maendeleo.

Tumechoka. Tunataka kuyafukuza madege haya tai , amesema Achel mfuasi wa chama cha FNL katika mkutano wa kampeni, akikumbushia shutuma za ulaji rushwa uliokithiri pamoja na upendeleo katika duru za utawala.

Hatua za amani ambazo zimekuwa zikifanyika tangu kumalizika kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Burundi vilivyochukua muda wa miaka 13 katika mwaka 2006 kwa kiasi kikubwa zimefanikiwa lakini wachunguzi wengi wanashaka kuwa joto hili la uchaguzi linaweza kuleta hali ya kuchemka.

Wakati hakuna hofu ya kuzuka tena mzozo baina ya makabila , matarajio ya mpambano wa uchaguzi kati ya makundi hasimu ya kisiasa yanayotaka kuungwa mkono na wapiga kura wa Kihutu kunaweza kudhoofisha zoezi hili la kidemokrasi nchini Burundi na kupelekea wapiganaji hao wa zamani kurejea tena katika mapambano , hali ambayo itavunja mafanikio yaliyopatikana hivi karibuni ya hatua za kuleta amani , imesema ripoti ya hivi karibuni ya kundi la kimataifa linaloangalia mizozo.

Muda wa kuelekea uchaguzi uligubikwa na ghasia kati ya makundi hasimu ya vijana pamoja na mauaji kadha ya kisiasa.

Mwandishi : Sekione Kitojo / AFPE

Mhariri: Abdul-Rahman