1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Inasema Azimio hilo halikupata ridhaa ya Burundi

Sylvia Mwehozi3 Agosti 2016

Serikali ya Burundi imekataa kupelekwa kwa polisi 228 wa Umoja wa Mataifa nchini humo ikisema kwamba azimio hilo lililoongozwa na Ufaransa lilifanywa bila ridhaa yake.

https://p.dw.com/p/1Jal4
Frankreich Geiselnahme Polizei in Rouen
Picha: picture-alliance/dpa/MAXPPP/J. Konitz

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa siku ya Ijumaa walikubaliana kupeleka kikosi cha polisi 228 nchini Burundi wakijaribu kumaliza mzozo wa zaidi ya mwaka mmoja wa vurugu.

Msemaji wa serikali ya Burundi Philippe Nzobonariba katika tamko lake amesema kwamba " serikali ya Burundi inakataa kila kipengele katika azimio hili linalohusishwa na kupelekwa kwa kikosi chochote katika ardhi yake", amesema Nzobonariba . Azimio la Umoja wa Mataifa lipo "katika ukiukaji wa kanuni za msingi zinazohitajika na Umoja wa Mataifa na zaidi ya yote kukiuka uhuru wake," aliongeza katika taarifa yake aliyoitoa jioni ya siku ya Jumanne.

Nzobanariba amesema kwamba azimio hilo la Umoja wa Mataifa linapaswa kupitishwa na nchi itakayoathirika na kwamba "bahati mbaya haikuwa hivyo". Ameongeza kwamba vikosi vya Burundi vilikuwa katika udhibiti wa hali ya ndani, na kwamba waangalizi 200 wa Umoja wa Afrika na wataalamu wa kijeshi bado wanakaribishwa. Burundi pia katika tamko lake imemshutumu jirani yake Rwanda kwa kuwaptia mafunzo waasi walio na silaha wanaoshambulia vikosi vya serikali mara kwa mara.

Wakati hayo yakitokea wiki iliyopita ujumbe wa serikali ya Burundi unatajwa kukwepa kikao maalumu cha kamati ya Umoja wa Mataifa kinachoshughulikia mateso cha kutathmini uwepo wa madai kwamba nchi hiyo inatekeleza mateso kwa raia pamoja na dhuluma nyingine.

Waandamanaji nchini Burundi
Waandamanaji nchini BurundiPicha: picture-alliance/dpa/D. Kurokawa

Kufuatia madai ya kuwepo kwa mateso na dhuluma nyingine dhidi ya raia wa Burundi zinazokiuka haki za binadamu, kamati ya Umoja wa Mataifa ya kushughulikia mateso iliandaa kikao maalumu cha kupitia madai hayo. Tarehe 28 Julai, ujumbe wa serikali ya Burundi ukiongozwa na waziri wa sheria Aimee Laurentine Kanyana uliweza kuhudhuria sehemu ya kwanza ya kikao hicho maalumu.

Katika hotuba yake, waziri huyo alisema kwamba sheria za Burundi zinakataa mateso na kwamba wale wanaohusika watawajibishwa. Waziri huyo alienda mbali zaidi kutaka kupuuzwa kwa ripoti zinazokuwa zimeegemea upande mmoja au zikitolewa na wapinzani wa kisiasa na kuitaka kamati hiyo kuzipuuza ripoti ambazo serikali ya Burundi haikupata nafasi ya kutoa maelezo.

Wajumbe wa kamati hiyo walitoa tuhuma mbalimbali ikiwemo mateso, mauaji ya kiholela, upoteaji, ubakaji na kuwachukulia hatua kali watetezi wa haki za binadamu na wanachama wa vyama vya upinzani huku wakiuliza maswali kadhaa dhidi ya hatua za serikali ya Burundi.

Hata hivyo siku ya pili ya kikao hicho, ujumbe wa Burundi haukuonekana popote. Mwenyekiti wa kamati hiyo alitangaza kwamba ujumbe wa Burundi ulituma taarifa ya kuomba muda zaidi wa kujibu.

Mwezi Julai pekee shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu la Human right watch lilichapisha ripoti mbili, moja ni kuhusu mateso yanayofanywa dhidi ya wale wanaoshukiwa kuwa wapinzani wa serikali na idara za kiusalama na polisi na nyingine ni inayohusu ubakaji unaofanywa na magenge ya vijana wa chama tawala.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi/AFP/HRW

Mhariri: Mohammed Khelef