1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rwanda yakanusha ripoti ya Refugee International

Admin.WagnerD15 Desemba 2015

Burundi imeshutumu tena Rwanda kwa kuunga mkono kundi la waasi ambalo linasajili wakimbizi wa Burundi nchini Rwanda, lakini Rwanda imekanusha.Hii inafuatia ripoti ya Refugee International iliyotolewa jana.

https://p.dw.com/p/1HNTQ
Burundi Gewalt ARCHIVBILD
Picha: picture-alliance/dpa/D. Kurokawa

Akizungumza na shirika la habari la Reuters, Willy Nyamitwe ambaye ni msemaji wa Rais wa Burundi, amesema nchi yake imekuwa ikisisitiza kuwa wakimbizi wa Burundi waliko kambini nchini Rwanda wamekuwa wakisajiliwa kujiunga na kundi la waasi, na kwamba Rwanda inawapatia mafunzo na silaha.

Pia msemaji huyo amesema kupitia ukurasa wake kwenye mtandao wa kijamii, kwamba kundi lenye silaha linaloongozwa na maafisa walioandaa jaribio la mapinduzi la mwezi Mei lililoshindwa, ambalo lililishambulia Burundi mwezi Julai, linapewa hifadhi nchini Rwanda. Nyamitwe amesema kundi hilo linaendelea kufanya kile alichokiita 'mashambulizi ya kigaidi dhidi ya Burundi'.

Shutuma hizo zimekuja baada ya shirika la kimarekani la kuwahudumia wakimbizi, Refugee International kuchapisha ripoti, ambamo limeelezea wasiwasi mkubwa kuhusu taarifa kwamba wakimbizi wa Burundi walioko Rwanda wanapatiwa silaha na kikundi ambacho sio cha kiserikali.

Wakimbizi walihojiwa

Shirika hilo ambalo limesema ripoti yake imetokana na mahojiano liliyoyafanya na wakimbizi, limezitaka Rwanda na Burundi kuheshimu misingi ya kibinadamu katika suala la wakimbizi, na kuwaepusha wakimbizi na usajili wa makundi yasiokuwa ya kiserikali.

Shutuma hizi zimekanushwa na Rwanda. Waziri wa nchi hiyo anayehusika na wakimbizi na kupambana na majanga Bi Seraphine Mukantabana, ameijibu Refugee Interanational kuwa shutuma hizo ni madai yasio na msingi wowote. Waziri huyo wa Rwanda amesema kuwa hata wakimbizi wachache wa Burundi wanaoamua kurudi nyumbani, hufanya hivyo kupitia njia zinazotambulika kisheria.

Bado hakuna maelezo ya kina yaliyotolewa, kuhusu sababu zinazoifanya Rwanda ambayo mwaka 1994 ilishuhudia mauaji ya kimbari yaliyoangamiza watu 800,000 wengi wao wakiwa kutoka jamii ya Watutsi, ingenuia kuliunga mkono kundi la waasi dhidi ya Burundi.

Wakimbizi wa Burundi wakiwa nchini Rwanda
Wakimbizi wa Burundi wakiwa nchini RwandaPicha: picture-alliance/AP Photo/E. Kagire

Haya ni matukio ya hivi karibuni ya uhasama kati ya nchi hizo jirani za Afrika, ambapo kila moja ina idadi ya kubwa ya watu wa kabila la wahutu na watutsi walio wachache.Nchi hizo zote zimekumbwa na mapigano ya kikabila na wataalamu wanahofu vita vinavyotokana na mzozo wa kisiasa kwa miezi sasa huenda vikasababisha madhara makubwa.

Zaidi ya 220,000 wahama Burundi

Zaidi ya watu 220,000 wamehama Burundi tangu mwanzoni mwa mwezi Aprili, kufuatia machafuko yaliyotokana na Rais Pierre Nkurunziza kuwania awamu ya tatu. Alichaguliwa tena kwenye uchaguzi uliokumbwa na utata mwezi Julai.Rwanda imesema zaidi ya warundi 73,000 wamekimbilia nchini humo.

Huku hayo yakiarifiwa, kesi dhidi ya waliofanya jaribio la mapinduzi mwezi Mei ilianza Burundi hapo jana. Zaidi ya majenerali 10 na maafisa wa kijeshi waliotuhumiwa kuhusika na jaribio la mapinduzi walifikishwa mahakamani nchini Burundi hapo jana mjini Gitega.

Aliyekuwa waziri wa ulinzi Cyrille Ndayirukiye na majenerali wengine watano ni kati ya watu wengine 28 ambao wameshtakiwa kwa kuhusika kwenye jaribio hilo la mapinduzi lililoshindwa.

Mwandishi:Bernard Maranga/DPA/Reuters

Mhariri: Gakuba Daniel