CAPE TOWN : Wanasayansi wataka waziri wa afya atimuliwe
6 Septemba 2006Zaidi ya wanasayansi 80 wa kimataifa wametuma baruwa ya wazi kwa Rais Thabo Mbeki wa Afrika Kusini kumtaka amtimuwe waziri wake wa afya kutokana na msimamo wake kwa suala la UKIMWI.
Manto Tshabala-Msimang kwa muda mrefu amekuwa akihoji faida ya kutumia madawa ya kurefusha maisha kwa waathirika wa UKIMWI na badala yake amekuwa akipigia debe matumizi ya kitunguu thomu,mafuta ya alizeti na limau kama dawa mbadala.
Wanasayansi hao wamesema kwenye baruwa iliyotolewa leo hii kwamba kutangaza sera zisizofaa na mbovu kuhusu HIV na UKIMWI kunahatarisha maisha na kuwa na mtu katika uwaziri wa afya ambaye hivi sasa haheshimiki kimataifa ni aibu kwa serikali ya Afrika Kusini.
Afrika Kusini ina watu wanaokadiriwa milioni 5 na nusu wanaoishi na virusi vya HIV hiyo ikiwa ni idadi kubwa kabisa duniani ikitanguliwa na India.