1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ceferin rais mpya UEFA

14 Septemba 2016

Aleksander Ceferin kutoka Slovakia alichaguliwa kuwa rais mpya wa shirikisho la kandanda la mataifa ya Ulaya UEFA leo Jumatano(14.09.2016) na kuchukua nafasi iliyoachwa wazi na Michel Platini na FIFA.

https://p.dw.com/p/1K1xp
Aleksandar Ceferin
Aleksander Ceferin rais mpya wa UEFAPicha: picture-alliance/AA/A. Beno

Ceferin mwenye umri wa miaka 48 , rais wa shirikisho la kandanda la Slovenia , alimshinda mpinzani wake pekee katika kinyang'anyiro hicho rais wa shirikisho la kandanda la Uholanzi Michael van Praag kwa wingi wa kura 42 dhidi ya 13 katika mkutano maalum wa UEFA mjini Athens.

Griechenland Aleksander Ceferin in Athen
Rais wa UEFA Ceferin katika mkutano wa UEFA mjini AthensPicha: picture alliance/dpa/EPA/Y. Kolesidis

"Sisi ni wadhamini wa mchezo huu murua," Ceferin alisema. Jukumu hili ni dira yangu na nataka kuweka wizani sawa baina ya wadau wote.

Jukumu kubwa kabisa la Ceferin ni pamoja na kutoa uhakikisho kwa vyama vidogo vya soka katika shirikisho la UEFA kuhusiana na mabadiliko ya hivi karibuni katika Champions League, ambayo yanapendelea nchi kubwa pamoja na hatua za kuomba kuwa mwenyeji katika mashindano ya mwaka 2024 ya kombe la mataifa ya Ulaya.

Platini alipigwa marufuku kushiriki katika shughuli zozote za kandanda kwa kile waendesha mashitaka wa Uswisi walichokieleza kuwa malipo ya kiasi ya faranga za Uswisi milioni 2 bila utaratibu wa kisheria , alizopokea kutoka kwa rais wa zamani wa FIFA Joseph Sepp Blatter mwaka 2011 kwa kazi alizofanya kama mshauri wa rais wa FIFA muongo mmoja uliopita.

Schweiz Michel Platini und Sepp Blatter
Michel Platini na Sepp Blatter Mei 29 , 2015.Picha: picture-alliance/dpa/W. Bieri

Ceferin sasa atakamilisha kipindi cha tatu cha miaka minne cha uongozi wa Platini, ambacho kinamalizika Machi 2019.

Van Praag hana jipya

Van Praag , alishindwa kuwashawishi wajumbe kwamba yeye anafaa kuiongoza UEFA na kuipeleka mbele.

Hotuba yake ya kabla ya uchaguzi haikuwa na mawazo ya kimapinduzi lakini alisema umri wake sio kikwazo, akieleza kwamba Mick Jagger na kundi la Rolling Stones wanaendelea kufanya ziara wakiwa na umri wa miaka zaidi ya 70.

Ceferin , ambaye ni mwanasheria, anapanga kujadili ukomo wa kipindi cha utawala na kuanzishwa kwa idara ya muafaka katika kipindi chake akiwa madarakani na alipinga shutuma kwamba hana uzoefu.

"Iwapo kila mara unasema sana kuwa unataka kuwa kiongozi, huenda wewe si kiongozi," alisema. "Mimi sio mtu wa kujionesha na si mtu wa ahadi ambazo haziwezekani."

Michel Platini
Michel Platini akiwahutubia wajumbe katika mkutano wa UEFA mjini AthensPicha: Getty Images/P. Schmidli

Na pia alisisitiza kwamba yeye si mtu tu wa mbele akiwaongoza watu wengine walioko nyuma ya pazia.

"Mara mimi ni kikaragosi wa rais wa FIFA Gianni Infantino, na siku ya pili ni mwanasesere wa Platini, siku nyingine ni mwanasesere wa Urusi. "Watu kwa kweli wana matatizo katika kuelewa kwamba mimi ni mtu huru."

Platini azungumza na wajumbe

Kabla ya uchaguzi Platini aliruhusiwa kutoa hotuba ya kuaga baada ya kupewa ruhusa maalum ya kuwahutubia wajumbe wa mkutano huo na shirikisho la kandanda duniani FIFA licha ya marufuku ya miaka minne kujihusisha na masuala ya michezo.

"Mtaendeleza ujumbe huu muhimu bila mimi," Platini aliwaambia wajumbe. "Nafsi yangu iko safi kabisa, sijafanya makosa na nitaendelea kupambana mahakamani."

Platini mwenye umri wa miaka 61, mchezaji nyota wa zamani wa Juventus Turin na timu ya taifa ya Ufaransa , hivi sasa anatarajiwa kuvunja uhusiano wa miongo kadhaa na mchezo wa kandanda.

Michael van Praag
Michael van Praag rais wa shirikisho la kandanda la UholanziPicha: Getty Images/D. Mouhtaropoulos

Hadi alipoporomoshwa na kashfa hiyo, alikuwa mmoja kati ya wagombea wa juu kuweza kuchukua nafasi ya Blatter kama mkuu wa FIFA, kazi ambayo hatimaye ilimwangukia katibu mkuu wa UEFA Gianni Infanitino.

Evelina Christillin , mtayarishaji wa michezo ya olimpiki ya majira ya baridi ya mwaka 2006 mjini Turin , alichaguliwa bila kupingwa kuwa mwakilishi mwanamke katika baraza la FIFA kutoka shirikisho la UEFA. Sheria mpya za FIFA zinasema kila shirikisho linapaswa takriban kuwa na mjumbe mmoja mwanamke katika baraza hilo.

Mwandishi: Sekione Kitojo /

Mhariri :Yusuf Saumu