1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Chad yataka Ufaransa ifunge kambi zake na kuondowa wanajeshi

1 Desemba 2024

Chad na Senegal zataka Ufaransa iondowe wanajeshi wake katika ardhi za mataifa hayo makoloni yake ya zamani.Rais Bassirou Faye asema Uhusiano kati ya Senegal na Ufaransa hauhitaji kuhusisha wanajeshi.

https://p.dw.com/p/4ncN5
Rais  Mahamat Idriss Deby Itno na Emmanuel Macron
Rais Mahamat Idriss Deby Itno na Emmanuel MacronPicha: Benoit Tessier/REUTERS

Serikali ya Chad imetangaza kufuta makubaliano ya kijeshi na kiusalama iliyokuwa nayo na koloni lake la zamani Ufaransa.

Uamuzi wa Chad unamaanisha wanajeshi takriban 1,000 wa Ufaransa watatarajiwa kuondoka katika taifa hilo la Afrika ya Kati.

Ni hatua ambayo inaonekana kama ishara ya kuzidi kufifia kwa ushawishi wa Ufaransa katika mataifa yaliyokuwa makoloni yake ya zamani.

Mbali na Chad rais wa Senegal Bassirou Diomaye Faye amesema wanajeshi wa Ufaransa wanapaswa kuondoka nchini mwake katika kipindi cha katikati  ya muhula wake.

Makabidhiano ya magari ya kijeshi aina ya ERC 90  kati ya Ufaransa na Chad
Ufaransa ikikabidhi Chad magari ya kijeshi aina ya ERC 90 mwaka 2021Picha: Renaud Masbeye Boybeye/AFP/Getty Images

Faye aliyasema hayo katika mahojiano aliyofanyika  na vyombo vya habari vya Ufaransa siku ya Ijumaa. Hakufafanua kuhusu tarehe ya kutaka hilo lifanyike lakini ameahidi kwamba Ufaransa itafahamishwa wakati sahihi.

Kimsingi, Ufaransa bado rasmi ina wanajeshi kiasi 350 ndani ya Senegal na rais Faye amesisitiza kwamba ushirikiano baina ya nchi yake na Ufaransa hauhitaji kambi za kijeshi za Ufaransa kuwepo Senegal.Soma pia: Kwanini Afrika Magharibi imekuwa kitovu cha ugaidi duniani?

Vyombo vya habari nchini Ufaransa, viliripoti wamba serikali mjini Paris toka hapo, ilitaka kuondoa mamia ya wanajeshi wake kutoka barani Afrika.

Waziri wa mambo ya nje Jean-Noël Barrot  alipangiwa kwenda Chad na Senegal ikiwa ni sehemu ya vituo vya ziara yake katika mataifa kadhaa ya kigeni.

Chad na Senegal zasema wakati umefika wa mamlaka huru

Maafisa wa Chad na Senegal wote wamesema ni wakati umefika wa mataifa yao kuangalia upya mahusiano yao na Ufaransa na  kwamba yanahitaji uhuru wa mamlaka yao.

Japo pia wizara ya mambo ya nje ya Chad imesisitiza nchi yake haihoji mahusiano ya kirafiki ya kihistoria na Ufaransa.Soma pia: Hatma ya vikosi vya Ufaransa Mali mashakani

Maandamano Niamey ya kupinga vikosi vya Ufaransa
Maandamano Niamey ya kupinga vikosi vya Ufaransa Sept 18 2022Picha: BOUREIMA HAMA/AFP/Getty Images

Itakumbukwa kwamba mambo yalikuwa tofauti na nchi kama Mali, Burkina Faso na Niger ambazo ziliigia kwenye mvutano mkubwa na Ufaransa baada ya mapinduzi ya kijeshi kwenye mataifa hayo matatu katika miaka ya hivi karibuni.

Mwamko wa kuipinga Ufaransa katika mataifa hayo unatiwa msukumo na kupata nguvu kutoka Urusi  ambayo imekuwa mshirika muhimu wa mataifa hayo.

Senegal inapakana na mataifa hayo upande wa  Magharibi na Chad upande wake wa Mashariki.

 

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW