Chad yafanya kura ya maoni kuamua kuhusu katiba mpya
17 Desemba 2023Sehemu kubwa ya upinzani pamoja na mashirika ya kiraia katika nchi hiyo ya Afrika ya Kati wanatowa mwito wa kususiwa mchakato huo.
Wanatowa hoja kwamba ni mpango uliotengenezwa kufungua njia ya kufanyika uchaguzi wa kumrudisha madaraka rais wa sasa wa mpito jenerali Mahamat Idriss Deby Itno na kuendeleza utawala wa kifamilia ulioanzishwa na marehemu baba yake miaka 33 iliyopita aliyeingia madarakani kupitia mapinduzi.
Kambi inayounga mkono kura hiyo ya maoni wana uhakika wa kupata ushindi baada ya kufanyika kampeni kubwa iliyogharimiwa na utawala wa kijeshi dhidi ya kambi ya upinzani iliyogawika na ambayo viongozi wake wengi walikamatwa,na kukabiliwa na vitisho kwa zaidi ya mwaka mmoja.
Picha za kuhamasisha raia wapige kura ya kuunga mkono rasimu ya katiba zimebandikwa kila sehemu katika mji mkuu N'Djamena.
Je, katiba mpya italeta mabadiliko nchini Chad baada ya msukosuko?
Rasimu hiyo ya katiba haina tofauti kubwa na katiba ambayo jeshi iliibatilisha mnamo mwaka 2021 na kuuweka utawala ulioyaweka madaraka makubwa kwa rais.
Kambi ya Upinzani inayopigia upatu utawala wa shirikisho uko upande usiounga mkono rasimu hiyo ya katiba katika mchakato huo wa kura ya maoni unaofanyika mpaka saa kumi na moja jioni ambapo vituo vya kupiga kura vitafungwa.
Matokeo ya awali ya kura hiyo yanatarajiwa kutangazwa Desemba 24 huku mahakama kuu ya nchi ikitakiwa kuyaidhinisha siku nne baadae.
Kambi ya upinzani na mashirika ya kiraia yanatarajia kwamba wito wao wa kuwataka raia wasusie utawafanya wengi kutojitokeza na pengine kuhujumu uhalali wa kura hiyo ya maoni.
Baadhi ya wanasiasa wa upinzani nchini humo lakini wanaamini matokeo tayari yanajulikana na rasimu hiyo ya katiba itaungwa mkono.
Chad itafanikiwa kurejea chini ya utawala wa kiraia uchaguzi ujao?
Mahamat Deby,mwenye umri wa miaka 37, alitangazwa rais wa mpito na jeshi mnamo mwaka 2021 kufuatia kifo cha baba yake Idriss Deby Itno aliyeuwawa na waasi akielekea kwenye uwanja wa mapambano nchini Chad.
Alipoingia madarakani aliahidi kuitisha uchaguzi baada ya kipindi chake cha mpito cha miezi 18 kumalizika na akatowa ahadi mbele ya Umoja wa Afrika kutokwenda kinyume.
Hata hivyo miezi 18 baadae serikali yake ikajiongezea muda madarakani kwa kipindi cha miaka miwili na kumruhusu kugombea uchaguzi wa rais uliopangwa kufanyika mwishoni mwa mwaka 2024.