1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Chama cha ANC chatafuta mkakati mpya wa sera za kuwaendeleza wananchi

Sekione Kitojo29 Juni 2007

Wanaharakati katika chama tawala nchini Afrika kusini cha African National Congress , ANC, wanaweka mbinyo ili serikali iingilie kati zaidi katika masuala ya uchumi, ikiwa ni pamoja na sheria ngumu zaidi zinazohusu makampuni ili kutoa msukumo zaidi katika maendeleo ya jamii pamoja na uchumi wa nchi hiyo. Hii ni katika mkutano mkuu wa chama hicho unaozungumzia masuala ya sera za chama mjini Midrand nchini Afrika kusini.

https://p.dw.com/p/CB3B
Bandera ya ANC
Bandera ya ANCPicha: AP

Katika ukosoaji wa hali ya juu kuhusiana na mafanikio ya serikali baada ya miaka 13 ikiwa madarakani, chama cha ANC kimesema , masuala kama utengenezaji wa nafasi za kazi, mageuzi ya sheria ya ardhi pamoja na elimu ya mbinu za kazi haviwezi kuachwa katika mikono ya soko la kazi.

Lakini watu wanaopanga mikakati pia wamesema kuwa seriali itawekeza katika ujenzi wa miundo mbinu ili kusaidia katika uimarishaji wa maendeleo ya uchumi. Tunakubaliana kuwa tunahitaji kujenga taifa lenye maendeleo , likiwa na uwezo wa kuingilia kati katika masuala ya uchumi kwa maslahi ya maendeleo ya taifa, kwa maslahi ya viwango vya juu vya ukuaji wa uchumi, lakini pia kwa maslahi ya ujumuisho wa jamii, mwanaharakati katika chama hicho Joel Netshitenzhe amesema katika siku ya pili ya mkutano huo kuhusu sera mjini Midrand, karibu na Johannesburg.

Serikali inahitajika kuangalia pia kuhusu njia za kuweza kuufanyia mageuzi uchumi ili kuhakikisha ushiriki zaidi ya watu wa kawaida wa nchi hii. Amesema.

Afrika kusini imo katika kipindi kirefu cha ukuaji wa uchumi ambao hauyumbi, lakini viwango ambavyo si rasmi vya watu wasio na ajira ni zaidi ya asilimia 40 na idadi ya watu ambao hawaridhishwi na hali hiyo inazidi kuongezeka kwasababu ya kupanuka zaidi kwa tofauti kati ya masikini na matajiri.

Mkutano huo wa siku nne ulianza siku ya Jumatano kufuatia mgomo mkubwa kabisa kuwahi kufanyika nchini humo wa wafanyakazi wa huduma za umma kuhusiana na ongezeko la mishahara tangu kuanguka kwa utawala wa kibaguzi mwaka 1994.

Mgomo huo , ambao ulianza Juni mosi, ulimalizika siku ya Alhamis wakati vyama vingi vya wafanyakazi vilipokubali nyongeza ya asilimia 7.5 ya mishahara kutoka serikali.

Tatizo ni kwamba nchini Afrika kusini tuna sekta ya juu kabisa ya ubepari ambayo imepiga hatua kubwa na ambayo inawabana watu wenye mitaji ya chini na kati kuweza kushiriki katika uchumi wa nchi hiyo, mjumbe wa kamati kuu ya taifa ya ANC Jeremy Cronin amesema.

Mjumbe mwingine akaongeza kuwa ANC haifurahishwi na hali ya mambo ilivyo hivi sasa.

Alama muhimu ya serikali yenye mtazamo mpya itakuwa mpango mkubwa wa miundo mbinu utakaowasilishwa na kuendeshwa na mashirika yanayomilikiwa na serikali.

Hatutoi ujumbe wa kitisho. Uingiliaji kati ni kufanya kile ambacho tunaweza kukifanya na kuamini kuwa kina manufaa kwa ajili ya watu wengi wa Afrika kusini ameongeza kusema Netshitenzhe.