Chama cha FDD kimeshinda uchaguzi Burundi
30 Julai 2005Bujumbura:
Chama kilichokuwa cha waasi wa Kihutu ambao ni wengi FDD kimeshinda uchaguzi wa Baraza la seneti uliofanywa jana katika hatua nyingine ya kuelekea kwenye amani ya kudumu nchini Burundi. Kushinda huko kulikokuwa kunatarajiwa kwa chama hicho kunamhakikishia Kiongozi wake, Pierre Nkurunziza kuwa Rais mwezi ujao. Uchaguzi wa Rais utafanywa kwa kufuata mwenendo wa kidemokrasia na kumaliza miaka 12 ya vita vya wenyewe kwa wenyewe. Mwenyekiti wa Tume ya uchaguzi, Paul Ngarambe, amesema kuwa chama cha FDD kimepata viti 30 kati ya 34. Chama tawala cha Wahutu FRODEBU kimechukua nafasi ya pili na kujipatia viti vitatu na mshirika wa FDD, CNDD kimepata kiti kimoja. Watwa watapewa viti vitatu na waliokuwa Marais wanne wa Burundi ambao ni hai kila mmoja atakuwa na kiti chake katika Baraza la Seneti lenye Wajumbe 41.