1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Champions League: Awamu ya makundi kufikia kikomo

9 Desemba 2013

Ligi ya Mabingwa UIaya inatarajia kushuhudia sarakasi za kila aina wiki hii, wakati awamu ya mechi za makundi ikifikia kikomo. Nafasi nane katika awamu ya timu 16 za mwisho bado ziko wazi. Ni nani atakayefuzu?

https://p.dw.com/p/1AVXi
Champions League Borussia Dortmund SSC Neapel
Picha: Reuters

Macho yote yanaangaziwa kundi F ambapo Napoli, Borussia Dortmund na Arsenal zinawania nafasi mbili. Huku Juventus na AC Milan kila mmoja akihitaji pointi moja ili kufuzu, dhidi ya wapinzani wagumu, huenda Italia ikawa na timu zake zote tatu katika awamu ya mchujo, au iambulie patupu kabisa. Nafasi za Benfica kufika fainali katika uwanja wao wenyewe wa Estadio da Luz haziko mikononi mwao tena, na zitakwisha kabisa kama Olimpiakos itawashinda Anderlecht, wakati wenzao Porto pia wakikabiliwa na mlima mkubwa.

Mabingwa wa Uswisi Basel, wanahitaji pointi tu ili kuendelea mbele, kama Schalke watashindwa. Shakhtar Donetsk, Bayer Leverkusen, Zenit St Petersburg na Ajax Amsterdam pia zina nafasi ya kufuzu. Manchester United, Real Madrid, Paris St Germain, Bayern Munich, Manchester City, Chelsea, Atletico Madrid na Barcelona tayari zilifuzu.

Champions League - FC Schalke 04 gegen Chelsea
Chelsea tayari wamefuzu lakini watalenga kuwapiku Staeua BucharestPicha: Martin Rose/Bongarts/Getty Images

Hivyo basi mambo yatakuwa hivi:

Arsenal (pointi 12) wanasafiri kucheza ugenini dhidi ya Napoli (9) wakihitaji sare, au kichapo kisichozidi magoli matatu, wakati Borussia Dortmund (9), wakiweza kufuzu kama watawashinda Olympique Marseille,bila kuzingatia matokeo mengine.

Kama Napoli na Dortmund zote zitashinda michuano yao, zitamaliza na pointi 12 sawa na Arsenal na hivyo uamuzi wa ni nani atakayefuzu utatokana na matokeo baina ya timu hizo tatu.

Kundi E pia litakuwa na sarakasi za aina yake, wakati Basel (pointi 8) watakamenyana na Schalke (7) wakihitaji pointi moja tu kujiunga na Chelsea katika awamu ya mchujo. AC Milan (pointi 8) lazima wapate pointi wanayohitaji dhidi ya Ajax Amsterdam (7) ili kujiunga na Barcelona kutoka kundi H.

beim Arsenal Spiel gegen Norwich
Mesut Özil ameongeza kasi katika safu ya ushambulizi ya ArsenalPicha: picture-alliance/dpa

Viongozi wa Serie A Juventus (6) watachuana na Glatasaray wakihitaji pointi moja katika kundi B, wakati Zenit St Petersburg (6) wakipigiwa upatu kuwafuata Atletico Madrid kutoka kundi G, wakati watakapomenyana na Austria Vienna katika mpambano wao wa mwisho.

Porto (pointi 5) wana safari ngumu dhidi ya Atletico, wakati Benfica na Olympiakos (zote na pointi 7) zikipambana kwa nafasi ya pili katika kundi C ambako Paris St Germain tayari wamefuzu. Olympiakos watakabana koo na Anderlecht huku Benfica wakiangushana na PSG.

Katika kundi A, ambapo Manchester United tayari wamefuzu, itakuwa na sarakasi za aina yake pia. Shaktar Donetsk (8) wako katika nafasi ya pili, lakini lazima wacheze Old Trafford huku Bayer Leverkzsen, ambao wana pointi moja nyuma, wakisafiri kuchuana na Real Sociedad ambao wana pointi moja pekee. Bayern Munich na Manchester City zitapimana nguvu tu kwa sababu timu zote tayari zimefuzu katika kundi D.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman