Champions League duru ya tatu yarejea viwanjani
16 Oktoba 2017Katika Champions League barani Ulaya kesho vumbi litatimka pale miamba wa Manchester City watakapokabana koo na Napoli ya Italia katika kundi F kesho Jumanne. Viongozi hao wa Premier League na Serie A wamekuwa wakitamba katika ligi zao wakifunga mabao wapendavyo.
Mara ya mwisho timu hizo kushindwa kupata ushindi katika ligi zao ni wakati City ilipotoka sare na Everton mwezi Agosti.
Katika michuano ya Ulaya , ni City ambayo ina rekodi nzuri kwa kuishinda Feyernood ya Uholanzi na Shakhtar Donetsk, wakati Napoli ilishindwa ilipokutana na mabingwa hao wa Ukraine. Kwa hiyo klabu hiyo kutoka Italia itakuwa katika mbinyo wa kupata matokeo mazuri wakati watakapokwenda mjini Manchester kupambana na City katika uwanja wa Etihad.
Msisimko mwingine uko katika kundi H ambapo mabingwa watetezi misimu miwili Real Madrid watakapokuwa wenyeji wa Tottenham Hot Spurs kesho Jumanne. Madrid na Tottenham wameshinda mara mbili kila mmoja na kuziweka Borussia Dortmund na APOEL Nikosia katika hali ya mashaka makubwa kuweza kufuzu kuingia katika timu 16 bora. Dortmund inasafiri kwenda Nikosia kupambana na APOEL timu zote zikiwa hazina pointi.
Mkurugenzi wa sporti wa Borussia Dortmund Michael Zorc amesema ushindi ni muhimu ili kufufua matumaini yao ya kuingia katika awamu ya mtoano ya timu 16 zitakazosalia. Kikosi cha kocha Peter Bosz kilipata kipigo cha kwanza nyumbani baada ya michezo 41 katika Bundesliga Jumamosi dhidi ya Leipzig ambayo nayo sasa inalenga kupata ushindi wake wa kwanza katika mashindano ya Ulaya wakati itakapokuwa wenyeji wa Porto ya Ureno katika kundi G kesho Jumanne.
Sevilla inaweza kubakia kiongozi wa kundi E itakapozuru Spartak Moscow kesho. Sevilla ina pointi nne, mbili zaidi ya Spartak na Liverpool.
Kudhibiti kimbunga cha mashambulizi cha Paris Saint Germain cha kina Neymar, Kylian Mbappe na Edinson Cavani ni mtihani mkubwa kwa safu ya ulinzi ya Anderlecht ya Ubelgiji siku ya Jumatano. Na PSG inaelekea kupata ushindi wake wa tatu katika kundi B.
Katika kundi hilo la B kuna pia Bayern Munich ambayo inakwaana na Celtic siku ya Jumatano, ikiwa chini ya kocha mpya Jupp Heynckes aliyeshawishiwa na viongozi wa Bayern kusitisha muda wake wa kustaafu na kuja kukinoa kikosi hicho.
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe / rtre / dpae / ape
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman