1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Champions League: Leverkusen na Bayern viwanjani

29 Septemba 2015

Timu mbili za Ujerumani zinaingia dimbani jioni hii katika mechi ya pili ya ligi ya mabingwa msimu huu.Bayern Munich inaikaribisha Dinamo Zagreb, huku Bayer Leverkusen ikiwa mgeni wa Barcelona isiyokuwa na Messi.

https://p.dw.com/p/1GfdC
Kikosi cha Leverkusen ambacho Leo Jumanne kinajipima kifua na Barcelona
Kikosi cha Leverkusen ambacho Leo Jumanne kinajipima kifua na BarcelonaPicha: Getty Images/A. Grimm

Mchezaji wa kiungo wa Bayer Leverkusen Christoph Kramer ameilinganisha firsa ya kucheza katika uwanja wa Barcelona wa Nou Camp kama ndoto iliyotimizwa. ''Tulifanya juhudi kubwa kufuzu kucheza katika Ligi ya Mabingwa msimu uliopita, na bila shaka tutaifurahia mechi'', amesema mchezaji huyo kijana wa miaka 24.

Ingawa kukosekana kwa Messi kutairahisishia Leverkusen, mkuu wa timu hiyo Rudi Voeller anasema wamesikitika, kwani mara zote hupendeza kumuona nyota huyo uwanjani.

Timu nyingine ya Ujerumani itakayojitosa uwanjani leo ni Bayern Munich ambayo imeshinda mechi zote 9 ilizocheza msimu huu, ambayo inaikaribisha Dinamo Zagreb ya Croatia, ambayo inajivunia kutopoteza mechi yoyote kati ya 45 ilizozicheza kabla ya ile ya leo.

Kiunzi kirefu

Hata hivyo, mbele ya Bayern Dinamo Zagreb inakabiliwa na kiunzi kirefu zaidi kukumbana nacho tangu rekodi yake hiyo ilipoanza kuhesabiwa.

Kocha wake Zoran Mamic anasema ni vizuri kujifariji kwamba wanaweza kucheza vyema zaidi leo, na kwa upande mwingine Bayern wakacheza ovyo zaidi ili waweze kuwafunga mabingwa hao wa Ujerumani.

''Kila kitu kinawezekana katika soka. Ikiwa tutacheza kama tulivyofanya dhidi ya Arsenal, tunaweza kupata matokeo mazuri'', amesema Mamic.

Nani wa kumzuia Lewandowski?

Lakini huu ni wakati ambapo nyota ya kikosi cha Bayern Munich kinachonolewa na Pep Guardiola inang'ara hasa. Jumamosi ilipata ushindi dhidi ya Mainz, na mshambuliaji wake Robert Lewandowski amekuwa moto wa kuotea mbali baada ya kutimiza magoli 101 katika ligi kuu ya Ujerumani, Bundesliga, zikiwemo mara tano alizotikisa nyavu katika muda wa dakika 9 tu.

Itakuwa kazi pevu kwa Dinamo Zagreb kumnyamazisha Robert Lewandowski
Itakuwa kazi pevu kwa Dinamo Zagreb kumnyamazisha Robert LewandowskiPicha: Getty Images/Alex Grimm

Beki wa Dinamo Zagreb Josip Josip amezungumza kiutani, kwamba ana matumaini Lewandowski hana magoli yaliyobakia baada ya mafanikio yake hivi karibuni.

Kocha wa Bayern Pep Guardiola amewaambia wandishi wa habari kwamba huenda asiwe na wachezaji wake mahiri, Arturo Vidal na Sebastian Rode ambao wanauguza majeraha, akisema anaweza kuwa na wachezaji 14 au 15 katika kikosi chake jioni hii.

Mwandishi: Daniel Gakuba/DW Website

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman