1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Champions League: Leverkusen yapoteza matumaini

19 Februari 2014

Mashindano ya Champions League barani Ulaya ikiwa ni duru ya mtoano ya timu16 bora imeanza jana (18.02.2014), wakati Bayer Levekusen ya Ujerumani ilipomenyana na PSG na Manchester City kutoana jasho na Barcelona.

https://p.dw.com/p/1BBIc
Champions League Leverkusen vs. Paris
Pambano kati ya Leverkusen na PSGPicha: Getty Images

Mapambano hayo hata hivyo hayakwenda kama ilivyotarajiwa. Nchini Ujerumani Bayer Leverkusen ilitarajiwa kujiweka katika nafasi nzuri ya kusonga mbele katika duru ya robo fainali na kutoa changamoto kubwa kwa kikosi kilichosheheni nyota wa kandanda kilichoundwa kwa mamilioni ya euro cha Paris St.Germain , lakini hali haikuwa hivyo. Leverkusen ilikubali kipigo cha mabo 4-0.

Champions League Leverkusen vs. Paris
Slatan Ibrahimovic akipongezwa na wachezaji wenzake wa PSGPicha: Getty Images

Huko Uingereza Manchester City ikicheza kwa mara ya kwanza katika awamu hii ya mtoani ya Champions League dhidi ya Barcelona ilitarajiwa kuwa mashabiki watashuhudia karamu ya magoli kutoka kila upande, lakini mchezo huo ulimalizika kwa ushindi wa mabao 2-0 kwa Barcelona.

Ibrahimovic ang'ara

Zlatan Ibrahimovic wa Paris St. Germain alipachika mabao mawili wakati kikosi hicho cha kocha Roland Blanc kilipojihakikishia tikiti yake katika robo fainali ya Champions League kwa ushindi wa mabao 4-0 ugenini wakati Bayer Leverkusen walimaliza mchezo huo wakiwa wachezaji 10 uwanjani jana Jumanne.

Champions League Leverkusen vs. Paris
Pambano kati ya Leverkusen na PSGPicha: Getty Images

Blaise Matuidi aliwapatia wageni hao wa Leverkusen bao la kuongoza katika dakika ya tatu tu ya mchezo huo. Ibrahimovic aliongeza bao la pili kwa mkwaju wa penalti katika dakika ya 39, baada ya Emir Spahic kumwangusha Ezequiel Lavezzi na kuoneshwa kadi ya pili ya njano, na kuwanyamazisha kabisa Leverkusen dakika tatu baadaye wakati alipopachika bao la tatu kwa mkwaju mkali nje ya eneo la hatari.

Spahic alitolewa nje kwa kadi nyekundu baada ya kupewa kati mbili za njano katika dakika ya 59.

Tulicheza vizuri , amesema Ibrahimovic , ambaye katika kinyang'anyiro cha Champions League msimu huu amepachika wavuni mabao 10.

Pellegrini awaka

Huko mjini Manchester mambo hayakuwa tofauti kwani Martin Demichelis wa Manchester City nae alitolewa nje kwa kadi nyekundu katika dakika ya 53 baada ya kuonekana amemwangusha mwenzake kutoka Argentina Lionel Messi katika eneo la adhabu.

Barcelona hakika inaonekana kufuta ndoto za Manchester City katika kombe hilo la Ulaya wakati ilipodhibiti mpambano huo wa awamu ya timu 16 katika bara la Ulaya na kupata ushindi wa mabao 2-0.

Kipigo hicho kilizusha maneno makali kutoka kwa kocha wa Man City Manuel Pellegrini ambaye alimshutumu mwamuzi kutoka Sweden Jonas eriksson kwa kuipendelea Barca na raia huyo wa Chile anakabiliwa na karipio na huenda adhabu kali kutoka shirikisho la soka la Ulaya UEFA.

"Nilizungumza nae mwishoni na kumwambia amefurahi kwasababu ameelekeza matokeo ya mchezo huo," Pellegrini amewaambia waandishi habari.

Champions League Manchester City vs. Barcelona
Martin Demichelis akimkata Lionel Messi na kuwa penaltiPicha: Getty Images

"Barcelona hawakuwa na nafasi ya kufunga hadi wakati wa mkwaju wa penalti dhidi ya Demichelis. Refa alikuwa anapendelea.Hakuwa na udhibiti kabisa katika mchezo huo. Nafikiri halikuwa wazo zuri kuwa na refa kutoka Sweden katika mchezo muhimu kama huo, amesema Pellegrini.

Alipoulizwa kwanini haikuwa sahihi kwamba Refa alitoka Sweden , alijibu : Michezo muhimu ya soka inachezwa katika eneo la Ulaya kuliko Sweden kwa hiyo mchezo mkubwa kama huo unaohusisha timu mbili muhimu, mchezo wa aina hiyo unahitaji refa mwenye uzoefu mkubwa.

Leo Champions League inaendelea kwa pambano kati ya mabingwa watetezi Bayern Munich ikiwa ugenini dhidi ya Arsenal London na pia AC Milan ikiikaribisha Atletico Madrid.

Mwandishi : Sekione Kitojo / rtre / ape