Champions League Ulaya na Afrika kutimua vumbi Jumanne
26 Novemba 2018Katika Champions League barani Ulaya vigogo vya soka vingi katika barani la Ulaya vinahitaji pointi moja tu kujihakikishia kuingia katika duru ya mtoano, lakini mbinyo wa Champions League unaikabili zaidi Paris Saint-Germain na Tottenham, wakati Bayern Munich ikihitaji kwa udi na uvumba msukumo zaidi. Vigogo vingi vitakuwa na matumaini kesho na keshokutwa kujiunga na Barcelona katika timu 16 zinazobakia katika Champions League , wakati nyingine zikitaraji kuepuka kuondolewa.
Mabingwa wa Ulaya Real Madrid, Manchester City, Bayern Munich , Roma, Juventus, Inter Milan na Porto zote zinahitaji pointi moja katika awamu hii ya makundi kufuzu.
Baadhi ya timu nyingine zitakuwa na matumaini ya kukata tikiti zao kwa ushindi, wakati timu kama Paris Saint-Germain , Tottenham Hotspur na Valencia zinapambana na hali zao.
Kundi C ni moja kati ya makundi ambayo timu zinakaribiana sana ambako Napoli itafuzu iwapo itaishinda Red Star Belgrade na PSG itashindwa kuiangusha Liverpool.
Hiyo ndio hali ya mambo katika kinyang'anyiro hicho ambapo kikosi cha Juergen Klopp kinatarji kukamilisha hatua hiyo kwa ushindi mjini Paris iwapo Napoli itaepuka kushindwa, lakini PSG , ambayo inamatumaini ya kuongezewa nguvu na wachezaji wake wa kati Neymar na mshambuliaji Kylian Mbappe , watakuwa wakipigania maisha yao.
Vigogo vya Afrika
Katika Bara la Afrika kuna mabingwa wa zamani watano wa Champions League barani humo miongoni mwa timu 52 zinazohusika katika kinyang'anyiro cha msimu wa mwaka 2018 / 19 kesho Jumanne na Jumatano. Orlando Pirates ya Afrika kusini na ASEC Mimosas ya Cote d'Ivoire zinaanza duru ya mwanzo kwa michezo ya nyumbani.
Ismailia ya Misri , Mamelodi Sundowns ya Afrika kusini na Club Africain ya Tunisia zina changamoto kubwa wakati zinasafiri kwenda katika mapambano yao. Mabingwa wengine watano mabingwa watetezi Esperance ya Tunisia, TP Mazembe na V Club za Jamhuri ya kidemokrasi ya Congo, Al Ahly ya Misri na Wydad Casablansa ya Morocco zimepita na kuingia katika duru ya pili.
Simba ya Tanzania inakwaana na Mbabane Swallows ya Eswatini zamani Swaziland, wakati Gor Mahia ya Kenya iko nyumbani ikiisubiri Big Bullets ya malawi. nayo Al Merrikh ya Sudan ni wenyeji wa Vipers ya Uganda. Al Hilal ya Sudan inapambana na JKU ya Zanzibar.
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe /rtre / ape / dpae
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman