Champions League uwanjani leo
2 Oktoba 2007Duru nyengine ya champions League-kombe la klabu bingwa barani ulaya inarudi uwanjani leo jioni:Mabingwa wa Ujerumani VFB Stuttgart wana miadi leo na FC Barcelona inayojivunia jogoo kama Ronaldinho.Mabingwa wa uingereza Manchester United pia wako nyumbani wakiwakaribisha AS Roma ya Itali.
Taarifa kutoka Munich zasema kuwa mshambulizi hatari wa timu ya taifa Miroslav Klose si fit kuteremka uwanjani hapo oktoba 13 pale Ujerumani itakapocheza na Ireland kuania tiketi ya finali za mwakani za Kombe la Ulaya.
Mabingwa wa Ujerumani Stuttgart wana kibarua kigumo leo nyumbani mbele ya FC Barcelona inayocheza na mastadi kama Ronaldinho.
Stuttgart haikuanza vyema msimu huu nyumbani na ikiwa leo itashindwa kutamba,huenda ikaambiwa buriani na mapema katika champions league.
Stuttgart itamtegemea zaidi mshambulizi wake hatari Mario Gomez,lakini mabeki mshahara wa Barcelona,wamekula kiapo kuwa hatafurukta.
Mpambano mwengine wa kusisimua jioni hii, ni kati ya mabingwa wa Uingereza Manchester United na AS Roma.
Msimu uliopita, timu za Uingereza pamoja na Manchester Utd. zilitamba awali mbele ya wataliana.Lakini ilikua AC Milan iliotoroka mwishoe na taji la kombe la Ulaya.Hatahivyo, Roma itabidi kuchunga vishindo vya Christiano Ronaldo na gengi lake usoni.
Kesho,duru hii itaendelea kwa makamo-bingwa Chelsea wakiumana na Valencia ya Spain.Chelsea wanaelewa vyema kwamba, wakishindwa kufua dafu kesho kutazuka balaa kubwa kwa kocha Avram Grant aliechukua usukani wa timu hii kutoka kwa Mreno Jose Mourinho.
Grant hakuanza vizuri kwani Chelsea, ililazwa mechi ya kwanza chini yake na Manchester United na baadae ikamudu suluhu tu na Fulham katika Premier League.
Liverpool ina miadi kesho na Marseille ya Ufaransa wakati Werder Bremen ya Ujerumani, itakuwa nyumbani kuwakaribisha wagiriki Olympiakos.Mabingwa wateteziAC Milan watakuwa Galsgow, Scotland kwa changamoto na Celtic.
Nje ya champions League,mshambulizi hatari wa Bayern Munich na mtiaji mabao mengi katika kombe lililopita la dunia,Miroslav Klose, si fit kuichezea Ujerumani Oktoba 13 itakapoania tiketi ya Kombe la Ulaya la Mataifa huko Uswisi,2008.
Ujerumani ina miadi siku hiyo na Ireland na siku 4 baadae na Jamhuri ya Czech.Kocha wa Bayern Munich Ottmar Hitzfeld amearifu kuwa Klose atakua nje ya chaki ya uwanja kwa wiki 3.
Mshambulizi wa klabu ya Uingereza ya Middlesbrough-Mido nae atakosa kuichezea Misri katika changamoto yake kali na Botswana mjini Cairo,Oktoba 13 kuania tiketi ya finali za mwakani nchini Ghana za kombe la Afrika la Mataifa.Mido nae ameumia.Mabingwa wa Afrika Misri, wanabidi kuepuka kushindwa na Botswana siku hiyo ili kutia mfukoni tiketi yao ya kwenda Accra.