Champions League yarudi tena uwanjani
2 Oktoba 2012Bayern Munich ina kibarua huko Belarus na BATE Borisov, wakati Barcelona na Benfica ya Ureno zinatiana kifuani. Huu ni mchezo wa duru ya pili katika awamu hii ya makundi katika Champions League katika bara la Ulaya.
Timu tatu za Ujerumani zilizomo katika kinyang'anyiro cha Champions League zimekuwa na mwanzo mzuri katika Champions League msimu huu. Vilabu vyote vimeweza kushinda katika mpambano wao wa mwanzo. Hivi sasa swali ni iwapo mwanzo huo mzuri utaendelezwa, licha ya kuwa katika michuano ya leo na kesho timu za Ujerumani zinakabiliwa na changamoto tofauti kabisa na wiki mbili zilizopita.
Ni Bayern itakayotimua vumbi
FC Bayern makamu bingwa wa ligi ya Ujerumani, Bundesliga, wana miadi mjini Minsk na BATE Borisov, wakionekana kuwa timu yenye uwezo mkubwa wa kupata ushindi, licha ya kuwa wenyeji wao wa Belarus huenda ukawa mchezo wao wa kwanza kupata ushindi.
Ushindi ni muhimu kwa Bayern Munich, licha ya kuwa itamkosa mshambuliaji wake wa pembeni Arjen Robben ambaye ni majeruhi.
FC Bayern ni timu pekee ambayo inaingia uwanjani miongoni mwa timu tatu zilizomo katika kinyang'anyiro cha Champions League msimu huu kutoka Ujerumani . Timu nyingine ni mabingwa wa Bundesliga , Borussia Dortmund na Schalke 04 ambazo zote zinakibarua hapo Jumatano.
Borussia ikipimana nguvu na mabingwa wa Premier League Manchester City na Schalke ikiwa nyumbani wakiwakaribisha mabingwa wa Ufaransa Montpellier.
Timu mbili zilizodhibiti kwa kiasi kikubwa ligi za nyumbani, zinakutana uso kwa uso leo.
Juventus Turin ya Italia inapambana na Shakhtar Donetsk, timu ambayo imeshinda michezo yake 25 iliyopita katika mashindano yote. Timu zote mbili ni mabingwa watetezi na viongozi wa sasa katika ligi zao za nyumbani. Hata hivyo kama zilivyo timu nyingine kutoka Ulaya mashariki Shakhtar , haijaweza kuonyesha makucha yake katika Champions League. Imeshawahi tu kufikia kiwango cha robo fainali misimu miwili iliyopita.
Mabingwa watetezi pia wamo
Kwa upande mwingine Nordsjaelland inakwaana na mabingwa watetezi wa Champions League Chelsea.
Licha ya hadhi yake ya kuwa mabingwa watetezi, Chelsea haiwezi kubweteka kwa kuwa imekwisha poteza points mbili nyumbani dhidi ya Juventus Turin wiki mbili zilizopita.
FC Barcelona ina miadi jioni ya leo na Benfica ya Ureno katika mchezo wa kundi G, ambapo pia katika kundi hilo , Spartak Moscow inachuana na Celtic Glasgow mjini Moscow. Manchester United iko nyumbani kwa CFR Cluj na kutoka katika kundi hilo Galatasaray ya Uturuki itaonyeshana kazi na Braga ya Ureno.
Kikosi cha Sir Alex Ferguson kimefanya kile kinachotarajiwa kwao kwa kuizamisha Galatasaray ya Uturuki katika mchezo wa kwanza katika kundi H uwanjani Old Trafford.
Mwandishi: Sekione Kitojo/rtre
Mhariri: Mohammed Khelef