Champions Ligi yaanza kutimua vumbi
12 Septemba 2017Ujerumani inawakilishwa na timu tatu , Bayern Munich , Borussia Dortmund pamoja na wageni katika ligi hiyo RB Leipzig.
Bayern Munich inajitupa katika uwanja wa Allianz Arena mjini Munich wakiwakaribisha Anderlecht ya Ubelgiji, jaribio ambalo halitakuwa na changamoto kubwa kwa kikosi hicho cha kocha Carlo Anceloti. Hali ya katika klabu hiyo kwasasa ni ya mawimbi, kutokana na matamshi ya mshambuliaji wa kutumainiwa wa klabu hiyo Thomas Muller kwamba kuna maisha hata bila Bayern Munich yanaleta hali ya shaka shaka kwamba mchezaji huyo ana nia ya kuihama Bayern pengine msimu ujao, kutokana na kutopata nafasi ya kucheza kila mara katika kikosi cha Anceloti.
Hata mshambuliaji mahiri wa Bayern Munich Robert Lewandowski ametumbukia katika mjadala mkubwa hapa Ujerumani baada ya kuikosoa sera ya klabu hiyo ya manunuzi ya wachezaji wapya. Lewandowski amekosoa sera hizo na kusema , klabu hiyo haijaweza hata kuvuka kiwango cha euro milioni 40 kununu wachezaji wapya na hali hiyo itaiacha klabu hiyo nyuma ikilinganishwa na vilabu kama Paris St. Germain, Barcelona, Real Madrid, Manchester United na vingine.
Lakini wachezaji hao wametakiwa kucheza kandanda katika klabu yao na sio kuropoka. Ni swali la kungoja na kuona iwapo Bayern itashinda kwa kishindo leo dhidi ya Anderlecht ndipo itakapoonekana iwapo kibarua cha Carlo Ancheloti haitaota majani.
Barca inajaribu tena
Fainali ya Champions League ya mwaka 2015 kati ya Barcelona na Juventus Turin ambapo , Barca waliirarua Juve kwa mabao 3-1 itakumbukwa tena leo jioni wakati timu hizo zitakapokipiga katika uwanja wa Camp Nou. Pambano la mwaka jana la robo fainali ambapo Juve iliibuka kidedea bado liko katika hisia za wachezaji na mashabiki wa Barcelona.
Manchester United imerejea katika makaazi yake ya kawaida katika Champions League na inakabiliana na timu bora kabisa katika bara la Ulaya. Man U imeshindwa kufuzu kucheza katika Champions League mwanzoni mwa kampeni ya kwanza kocha nyota Jose Mourinho alipochukua uongozi wa kikosi hicho lakini ushindi wao wa kombe la Ulaya msimu uliopita ulitosha kutoa ishara ya mambo yajayo. Man U inakumbana na basel ya uswisi jioni ya leo.
Michezo mingine ni kati ya AS Roma ikiikaribisha Atletico Madrid , timu iliyonusa fainali mara mbili dhidi ya Real Madrid na kushindwa katika muda wa miaka mitatu iliyopita. Chelsea inaikaribisha Qarabag timu ambayo nayo ndio kwanza inaonja hewa katika anga hilo la juu kutoka Azerbaijan. Benfica ya Ureno inaikaribisha ZSKA Moscow , na Olympiakos ya Ugiriki ni wenyeji wa Sporting Lisbon.
Macho yote kwa PSG
Lakini macho ya mashabiki yataelekezwa zaidi katika mtanange baina ya Celtic wakiwa wenyeji wa Paris St. Germain. Mchezo huo utavutia hisia za mashabiki kwa kutaka kuwaona Neymar ambaye hivi karibuni alikuwa katika kila chombo cha habari baada ya kuitupa mkono FC Barcelona na kujiunga na timu hiyo iliyonununuliwa na kampuni ya uwekezaji wa Qatar. Mapambano yanaendelea hapo kesho kwa kundi jingine la timu 16 kupambana. RB Leipzig inaikaribisha AS Monaco ya Ufaransa, wakati Borussia Dortmund itakuwa mjini London katika uwanja maarufu wa Wembley wakipambana na Tottenham Hot Spurs. Kila la kheri.
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe /rtre /dpae
Mhariri: Yusuf , Saumu