1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Djinnit ziarani Maziwa Makuu

Saleh Mwanamilongo28 Agosti 2014

Mjumbe mpya wa Umoja wa Mataifa kwa Kanda ya Maziwa Makuu, Said Djinnit, ameanza ziara kwenye mataifa hayo akiahidi kushirikiana na viongozi wa huko kuimarisha uhusiano na kukuza imani baina yao.

https://p.dw.com/p/1D31u
Mjumbe Maalum wa Umoja wa Mataifa kwa Kanda ya Maziwa Makuu, Said Djinnit (kulia).
Mjumbe Maalum wa Umoja wa Mataifa kwa Kanda ya Maziwa Makuu, Said Djinnit (kulia).Picha: AP

Djinnit, ambaye leo anatazamiwa pia kukutana na Rais Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, ameitoa mjini Kinshasa ambako amewasili kwa mara ya kwanza tangu kuteuliwa kwake kushika wadhifa huo.

Mjumbe huyo mpya anachukuwa nafasi iliyochwa na mtangulizi wake Mary Robinson ambae hivi sasa amekuwa mjumbe wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Mabadiliko ya Tabianchi.

Djinnit alikutana kwanza na Waziri wa Mambo ya Nje wa Kongo, Raymond Tshibanada, akisema kuwa lengo la ziara yake ni kuwahakikishia viongozi wa Kongo kwamba atafanya na kazi ili kwa pamoja wahakikishe panakuwa na amani kwenye kanda hiyo ya Maziwa Makuu.

"Nimekuja ili kufanya kazi kwa pamoja, ili maswala kadhaa yapige hatua mbele katika njia nzuri kwa manufaa ya kanda nzima na kwa manufaa ya Kongo, na kwa ajili ya amani, usalama na ustawi wa kanda hii," alisema Djinnit, akiongeza kwamba juhudi za viongozi wa kanda hiyo katika kutafuta amani zitasaidiwa na kuungwa mkono na Umoja wa Mataifa.

Kongo yasisitiza kutimizwa kwa Mkataba wa Addis Ababa

Tshibanda alielezea kwamba cha muhimu kwa sasa ni kila nchi kutekeleza mkataba wa Addis Ababa kwa ajili ya amani. "Tunategemea uzoefu wake kwa ajili ya kupiga hatua mbele katika yale tunayoyafanya mnamo siku hizi, yaani kurejesha amani na ustawi kwenye kanda hii kupitia mkataba wa amani wa Addis Ababa na utekelezwaji wa majukumu ambayo kila upande uliyachukuwa."

Waziri wa Mambo ya Nje wa DRC, Raimond Tshibanda.
Waziri wa Mambo ya Nje wa DRC, Raimond Tshibanda.Picha: DW/J.Kanyunyu

Ziara hii itampeleka Djinnit pia nchini Rwanda, Tanzania, Angola, Afrika ya Kusini na Uganda. Mjumbe huyo alilisifu eneo la Maziwa Makuu kuwa "lina vyanzo vingi vya kujiendeleza na kuendeleza bara zima la Afrika."

"Nitafanya jitihada huku nikuomba ushauri kwa viongozi wa nchi za kanda hii katika kuheshimu ardhi ya kila nchi na vile vile kukuza imani baina ya mataifa haya, kwa sababu pasina imani hiyo, hakuna kitakachofanikiwa kwa pamoja. Kuna umuhimu wa kuanzisha miradi ya pamoja ya maendeleo," alisema Djinnit.

Baraza la Usalama lataka FDLR waweke silaha chini

Ziara hiyo imekuja siku moja tu baada ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kutoa taarifa ikionesha wasiwasi wake kuhusu kuzembea kwa taratibu ya kujisalimisha kwa wapiganji wa Rwanda wa FDLR.

Mmoja wa wapiganaji wa FDLR nchini Kongo.
Mmoja wa wapiganaji wa FDLR nchini Kongo.Picha: DW/S. Schlindwein

Baraza hilo limeiomba serikali ya Kongo na Kikosi cha Umoja wa Mataifa nchini humo (MONUSCO) kuzidisha shinikizo la kijeshi dhidi ya viongozi wa wapiganaji hao ambao wamekataa kutua chini silaha.

Hata hivyo, Baraza hilo lilielezea kwamba linadhani ilani ya miezi sita iliyotolewa na nchi za Maziwa Makuu na Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiuchumi Kusini mwa Afrika (SADC) kwa ajili ya waasi hao kutua chni silaha kwa hiyari yao wenyewe itatakelezwa.

Mwandishi: Saleh Mwanamilongo/DW Kinshasa
Mhariri: Mohammed Khelef