1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Dortmund ina kibarua katika Champions League

25 Novemba 2013

Timu kadhaa zinatarajiwa kujiunga na Barcelona, Bayern Munich, Manchester City na Atletico Madrid katika droo ya awamu ya timu 16 za mwisho katika Champions League baada ya mechi za raundi ya tano kukamilika

https://p.dw.com/p/1AOSt
DORTMUND, GERMANY - NOVEMBER 23: Eric Durm of Dortmund looks dejected after the second Munich goal scored by Arjen Robben during the Bundesliga match between Borussia Dortmund and FC Bayern Muenchen at Signal Iduna Park on November 23, 2013 in Dortmund, Germany. (Photo by Dennis Grombkowski/Bongarts/Getty Images)
Fußball Bundesliga Borussia Dortmund FC Bayern MünchenPicha: Getty Images

Real Madrid, Chelsea na Paris St Germain zinahitaji tu pointi moja ili kusonga mbele wakati ushindi wa Manchester United na Arsenal huenda ukazisaidia timu hizo kujiondoa katika awamu ya makundi na kufuzu katika awamu ya mchujo.

Baada ya kufungwa magoli matatu kwa sifuri na Bayern Munich katika mchuano mkubwa wa “der Klassiker”, Borussia Dortmund sasa wanakabiliwa na mtihani wa kufa kupona dhidi ya Napoli kesho Jumanne katika Champions League. Nao Bayern wanacheza Jumatano dhidi ya CSKA Moscow wakiwa wamejiamini kabisa kwa sababu tayari wamefuzu katika awamu ya mchujo.

Ushindi dhidi ya Moscow utahakikisha kuwa Bayern wanamaliza kileleni mwa kundi D. Na mengi yamezungumzwa sana kuhusu namna Mario Götze alivyoingia kama mchezaji wa akiba na kuubadilisha mchezo wa Jumamosi dhidi ya timu yake ya zamani Dortmund. Götze hata hivyo alionyesha heshima kwa kutoshangilia goli lake, na amekiri kuwa alikuwa na wakati mgumu kucheza kwa sababu kila mara alizomewa na mashabiki wa klabu yake ya zamani.

Mario Götze baada ya kufunga goli dhidi ya klabu yake ya zamani Borussia Dortmund
Mario Götze baada ya kufunga goli dhidi ya klabu yake ya zamani Borussia DortmundPicha: Reuters

Dortmund waliweza kuizuia kasi ya Bayern, kwa zaidi ya saa moja, lakini wakashindwa kuimarisha safu ya ulinzi, na hivyo kumpa Götze nafasi ya kupenya. Hilo anakubaliana nalo mlinda lango wa Dortmund Roman Weidenfeller

Bayern sasa wanaonekana kuwa kwenye mkondo wa kushinda taji la Bundesliga na pia katika nafasi nzuri ya kushinda kombe la Shirikisho, na pia Champions League. Kama tu wataendelea na mbinu yao ya ushindi katika vinyang'anyiro vyote vitatu, na hivyo kumpa kocha Pep Guardiola sifa ya kukikarabati kifaa ambacho hakikuwa kimevunjika sehemu yoyote.

Guardiola ni mwenye hasira

Lakini licha ya ushindi huo wa Jumamosi, Guardiola aliyeonekana kuwa mwenye hasira, ametishia kumtambua mtu ambaye amedai kuwa anafichua siri za mbinu za kiufundi za klabu na kutoa kwa vyombo vya habari. Amenukuliwa na gazeti la Bild akiwaambia wachezaji wake baada ya mechi dhidi ya BVB, kuwa “haijalishi ni nani, bila shaka mtu atawajibika”. Amesema “nitamrusha nje. Hatacheza tena katika kikosi changu”.

Kocha wa Bayern Munich Pep Guardiola
Kocha wa Bayern Munich Pep GuardiolaPicha: picture-alliance/dpa

Vijana wa kocha Jurgen Klopp ni kama wataziweka kando ndoto zao za taji la Bundesliga. Kikosi kimeathirika na majeruhi na lakini sasa wana kibarua cha kujaribu kuyaweka mambo sawa katika Champions League. Kwa sasa wako katika nafasi ya tatu ya kundi F, pointi tatu nyuma ya Arsenal na Napoli, na watakuwa wenyeji wa Napoli kesho. Kama watashindwa, basi ni kama watashuka katika daraja ya Europa League.

Basel inawakaribisha Chelsea, wakati Arsenal ikipambana na Marseille. Man United inachuana na Bayer Leverkusen. RealMadrid inawaalika Galatasaray Jumatano, wakati Barcelona wakishuka dimbani na Ajax. Nao Atletico wanasafiri kumenyana na Zenit St. Petersburg kesho Jumanne. Paris Saint-Germain itaangushana na Olympiakos siku ya Jumatano, wakati nao JUVE wakipambana na FC Copenhagen kesho Jumanne.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/Reuters

Mhariri: Yusuf Saumu