1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Dortmund, Manchester United zajiweka pazuri

Admin.WagnerD14 Februari 2013

Mechi za Ligi ya mabingwa barani Ulaya, Champions League, zilizochezwa jana (13.2.2013) baina ya Borussia Dortmund iliyokuwa na miadi na Shakhtar Donetsk, na Real Madrid na Manchester United ziliishia kwa sare.

https://p.dw.com/p/17dnA
Picha: Reuters

Mchezo baina ya Dortmund dhidi ya Shakhtar Donetsk ulimalizika kwa bao 2-2. Mlinzi wa Dortmund Mats Hammel ndiye aliyefanya mambo kuwa mazuri kwa timu yake baada ya kuitumia vizuri kona iliyopatikana dakika tatu kabla ya kupulizwa kipenga cha mwisho katika mchezo huo.

Dortmund yaponea chupuchupu

Kabla ya hapo mambo hayakuwa mazuri kiasi cha kuwafanya mashabiki wa kandanda kudhani kuwa hiyo ndiyo safari ya kumalizwa kwa ndoto za Dortmund kwenye mashindano hayo.

Baada ya kuiwezesha timu yake kusonga mbele, Hammels alisema " Ni muhimu kuwa tutaingia duru ya pili na hata tukipata sare ya 0-0 bado tutasonga mbele na mashindano".

Hammels alizungumzia mambo yalivyokuwa wakati wa mchuano na kusema kuwa walikabiliwa na vipindi vya hatari baadhi ya wakati hasa kwa upande wa safu ya ulinzi, lakini akasema pia kuwa hilo haliwezi kuepukika hasa ukizingatia mtindo wa mashambulizi wa Shakhtar.

Luiz Adriano wa Shakhtar(kushoto) akiwania mpira na Mats Hummels wa Borussia Dortmund kwenye mechi ya jana (13.2.2013)
Luiz Adriano wa Shakhtar(kushoto) akiwania mpira na Mats Hummels wa Borussia Dortmund kwenye mechi ya jana (13.2.2013)Picha: Reuters

Mpira wa kichwa uliowekwa nyavuni na mchezaji huyo umeiweka kwenye nafasi nzuri Dortmund ya kufika robo fainali ya mashindano ya Champions League. Mkufunzi wa Dortmund Jugen Klopp alisema baada ya mchezo huo kuwa waliadhibiwa kwa makosa yao kwenye safu ya ulinzi ambayo hata hivyo yalikuwa yanakera. Ushindi wa bao 2-1 usingekuwa kitu kibaya kwao lakini huu wa 2-2 ni muhimu zaidi kwa timu kabla ya kuingia duru ya pili.

Kwa upande wake Mkufunzi wa Shakhtar Mircea Lucescu amesema kuwa kwa sare hiyo ya 2-2 ni sawa na wameshindwa na kuwa hayo ni matokeo mabaya kwao. "Inasikitisha kupoteza kupoteza mwelekeo dakika za mwisho lakini matokeo hayo ni ya haki kabisa" alisema Lucescu.

Man U kicheko

Katika mechi baina ya Rael Madrid na Manchester United vigogo hao wa soka na pia waliishia sare ya bao 1-1 kwenye dimba la Bernabea . Kama ilivyo kwa Dortmund, Man U nayo imejiweka katika nafasi nzuri ya kuinusa robo fainali.

Cristiano Ronaldo wa Real Madrid katika mechi yao dhidi ya Man United
Cristiano Ronaldo wa Real Madrid katika mechi yao dhidi ya Man UnitedPicha: Reuters

Cristiano Ronaldo aliifungia Real bao la pekee katika mchezo huo. Man U walicharuka na kufanya mambo pale mpira wa kona uliopigwa na Wayne Rooney kufika miguuni mwa Danny Welbeck ambaye hakufanya ajizi na kuuweka kimyani mnamo dakika ya 20.

Ronaldo alisema kuwa wangelikuwa na nafasi tena dhidi ya Man U katika mchezo wa marudiano Old Trafford lakini ndo hivyo mambo hayakuwa mazuri. Kocha wa Manchester Sie Alex Ferguson aliuelezea mchezo huo kuwa ulikuwa mgumu na kukiri kuwa Real ni timu imara lakini akaongeza kuwa walicheza vizuri na walistahiki kupata mabao zaidi ya hilo moja.

Ajali ya ndege ya Donetsk

Hata hivyo huko Donetsk licha ya Dortmund kupata nafasi nzuri lakini mchezo huo uliingia dosari kutokana na vifo vya mashabiki watano wa kandanda walifariki dunia na wengine 12 kujeruhiwa baada ya ndege aliyokuwa wamepanda kutoka Odessa kusini mwa Ukraine iliyokuwa imebeba watu 45 ilipopata ajali wakati wa kutua katika uwanja wa ndege wa Donetsk.

Ajali hiyo ilitokea muda mfupi kabla ya kuanza kwa mchezo baina ya Dortmund na Shakhtar na inaaminika kuwa wengi wa watu hao walikuwa ni mashabiki wa kandanda waliokuja mjini humo kushuhudia mechi hiyo. Kabla ya kuanza kwa mchezo timu zote mbili zilisimama kwa dakika moja kuwaombea marehemu. Kutoka viwanjani sina la ziada..

Mwandishi: Stumai George/Dpa/Afp/Ape

Mhariri: Josephat Charo