Dortmund na Bayern nani mbabe?
12 Mei 2012Kocha wa Borussia Dortmund , Jurgen Klopp amesema kuwa anajisikia fahari kuiongoza timu yake katika uwanja ambao anahisi ni kama tukio linalotokea kila mwaka nchini Uingereza katika uwanja wa Wembley, katika kombe la FA. Nimekuwa naota ndoto kama hii tangu nikiwa kijana, kwangu mimi ni kama naingia Wembley. Tutacheza kama vile tupo Wembley , amesema Klopp, katika mkutano na waandishi habari siku ya Ijumaa wakati akijitayarisha kwa mara ya kwanza kuiongoza timu anayoifunza kuingia katika fainali yake ya kwanza ya kombe la DFB katika uwanja huo wa Olimpiki mjini Berlin.
Kocha wa Bayern Munich Jupp Heynckes anataka kwa udi na uvumba kulinyakuwa kombe hilo na kumaliza ubabe wa Borussia Dortmund dhidi ya Bayern kwa misimu miwili mfululizo. Mabingwa hao mara mbili mfululizo wa Bundesliga Borussia Dortmund wameishinda Bayern mara nne mfululizo katika ligi na wanamatumaini kuwa vijana wa Henckes watakuwa wanafikiria zaidi fainali ya Champions League wiki ijayo dhidi ya Chelsea badala ya kuweka ajili zao zote katika mchezo huo.
Nani ataibuka mbabe ni suala la kusubiri na kuona.
Chelsea hawana sababu ya kuhofia wakati watakapokutana na Bayern Munich katika fainali ya kombe la mabingwa mabarani Ulaya, Champions League wiki ijayo wakati ushindi wao katika nusu fainali ya kombe hilo dhidi ya Barcelona imethibitisha kuwa wanaweza kushinda timu bora katika bara la Ulaya , amesema hayo kocha mlezi Roberto Di Matteo.
Chelsea ni timu inayoonekana kuwa haina uzito wa kutosha wakati ikiingia katika fainali hii katika uwanja wa Allianz Arena mjini Munich wakati wakijaribu kuwa mabingwa wa Ulaya kwa mara ya kwanza katika historia.
Lakini Di Matteo , ambaye amebadilisha majaliwa ya klabu hiyo tangu aliposhika wadhifa huo kutoka kwa kocha mtangulizi wake Andre Villas Boas March mwaka huu, amesema kuwa wachezaji wake wanajisikia wenye matumaini.
Chelsea wanatambua kuwa iwapo hawataishinda Bayern katika fainali hiyo hawatashiriki katika champions League msimu ujao kwa kuwa hawawezi kumaliza katika nafasi zaidi ya sita katika ligi ya Uingereza , Premier League.
Chelsea imefanya vibaya katika ligi msimu huu , ambapo watamaliza nje ya timu bora nne za juu kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2002, na hali hiyo imesababishwa na fainali ya kombe la FA ambapo Chelsea ilipata ushindi dhidi ya Liverpool na sasa huenda wakapata ushindi dabali katika vikombe iwapo watanyakua Champions League na utakuwa ushindi wao mkubwa kabisa katika historia.
Kesho Jumapili ndio siku ya kukunja janvi la ligi ya Uingereza, Premier League, ligi ambayo imekuwa na mabadiliko ya ajabu na huenda italeta mshangao mwingine mkubwa kesho , iwapo Queens Park Rangers wataweza kuleta tafrani na kupata ushindi dhidi ya Manchester City. Taji lilikuwa linaelekea kwa kikosi hicho kinachovaa jezi za rangi ya maji ya bahari , wakati City ilipokuwa ikiongoza kwa points tano dhidi ya Manchester United miezi miwili iliyopita. Lakini Manchester City iliporomoka katika mwezi uliofuatia , na kuwaruhusu mahasimu wao wa Manchester United kufuta pengo hilo na kuongoza kwa points nane dhidi ya majirani zao hao.
Halafu ikawa zamu ya United kuporomoka katika mwezi uliofuatia , na City ikaja juu tena kwa wingi wa magoli dhidi ya mabingwa watetezi United, hadi kufikia mwisho wa ligi hiyo kesho.City inaweza kunyakua ubingwa wake wa kwanza wa Premier League tangu mwaka 1968 kwa kuishinda QPR, huku ubingwa ukiamuliwa kwa tofauti ya magoli kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1989 iwapo United nayo itaishinda Sunderland.
Lakini United iko tayari mdomo wazi kungojea City wanyang'anywe tonge kinywani na QPR, wakitambua kuwa hali hiyo itawaletea ubingwa wao wa 20. Mbio za kuwania ubingwa ziko hai hadi katika mchezo wa mwisho wa 38 katika Premeir League, huko Uingereza.
Timu ya taifa ya Tanzania imepata kocha mpya siku ya Ijumaa, kwa jina la Kim Poulsen kutoka Denmark. Kocha wa zamani Jan Paoulsen amemaliza muda wake wa miaka miwili na shirikisho la kandanda nchini Tanzania limeamua kutourefusha mkataba huo.
Nayo klabu ya Dar Young Africans ya mjini Dar Es Salaam imo katika mtihani mkubwa wakati ikikabiliwa na mgogoro mkubwa kabisa kuwahi kuikumba klabu hiyo kongwe nchini Tanzania. Wanachama na mashabiki wa timu hiyo wanataka uongozi wa juu wa klabu hiyo ujiuzulu. Hii inatokana na matokeo mabaya katika msimu huu ambapo klabu hiyo kongwe imemaliza ikiwa nafasi ya tatu nyuma ya mabingwa Simba Sports Club na Azam FC zote za Dar Es Salaam. Pia kipigo cha mabao 5 kwa nunge dhidi ya watani wao wa jadi Simba Sports Club katika mchezo wa kufunga msimu wiki iliyopita .
Riadha.
Riadha mwanariadha wa mbio za masafa marefu wa Ethiopia Kenenisa Bekele alituma ujumbe mkali kwa mahasimu wake katika mashindano ya Olimpiki kwa kusema kuwa analenga kushiriki katika mbio za mita 5,000 na 10,000 katika mashindano hayo jijini London.
Bekele ambaye ni bingwa wa Olimpiki na anayeshikilia rekodi ya ulimwengu katika mbio hizo mbili, amekuwa akisumbuliwa na maumivu katika kipindi cha miaka miwili iliyopita , lakini ametangaza kuwa yuko katika hali shwari bila maumivu , ijapokuwa hajaanza mazoezi kikamilifu.
Mwanaridha huyo mwenye umri wa miaka 29, ambaye anashikilia mataji 16 ya ulimwengu, aliweza kutimka mbio hizo mara moja tu mwaka 2010 na mara mbili katika mwaka wa 2011 wakati akijaribu kupuuzia maumivu aliyokuwa nayo ya goti.
Alipata matokeo mabaya zaidi katika mashindano ya ubingwa wa ulimwengu kule Daegu Korea Kusini mwaka jana, na kuchechemea akiondoka katika mbio za mita 10,000 na hata kujiondoa katika kikosi cha mbio za mita 5,000.
Lakini alirejea kwa kishindo na kuandikisha muda wa kasi zaidi katika mbio za mita 10,000 za msimu wa 2011 kwenye fainali ya Diamond League mjini Brussels mwezi Septemba, mbio anazosema zilimpiga jeki kabla ya mazoezi yake ya msimu wa baridi.
Ndondi.
Shirikisho la ndondi nchini Uingereza limeshutumu vikali pambano la kinyongo kati ya bingwa wa zamani wa masumbwi wa uzito wa juu David Haye na Dereck Chisora na kutishia kuweka vikwazo kwa yeyote anayehusika katika pambano hilo. Liseni ya Chisora katika ndondi n iliondolewa kabisa na bodi ya udhibiti wa mchezo wa ngumi nchini Uingereza March mwaka huu baada ya wanamasumbwi hao kuchapana kavu kavu wakati wa mkutano na waandishi habari kufuatia Chisora kushindwa katika pambano dhidi ya bingwa wa sasa wa dunia Vitali Klitschko mjini Munich Ujerumani mwezi wa Februari mwaka huu. Haye hana liseni kwa sasa kuweka kuzichapa ndondi nchini Uingereza baada ya kutangaza kustaafu mwaka jana baada ya kushindwa na Vladimir Klitschko.
Mwandishi : Sekione Kitojo /afp/rtre/ape/dpae
Mhariri : Othman Miraji