Dortmund ndio miamba ya Ujerumani
14 Mei 2012Nyota wa Japan Shinji Kagawa aliendelea kuufunga mdomo kuhusu hatima yake baada ya kufunga bao katika fainali hiyo. Mkufunzi wa Manchester United Alex Ferguson alikuwa katika uwanja wa michezo ya Olimpiki mjini Berlin na kumwona Kagawa akifunga bao la kwanza na kuandaa la pili lililofungwa na Robert Lewandoski ambaye alifunga matatu.
Kagawa ana mwaka mmoja uliosalia katika mkataba wake lakini hajaficha hamu yake ya kutaka kuhamia ligi ya Uingeerza huku United wakionekana kuongoza orodha ya wale wanaommezea mate. Nyota huyo wa Japan mwenye umri wa miaka 23 amefunga mabao 17 msimu huu katika vinyanganyiro vyote na kuisaidia Dortmund kushinda ligi kwa msimu wa pili mfululizo na kushinda mataji mawili kwa mara ya kwanza katika historia yao ya miaka 103.
Kocha wa Dortmund Jurgen Klopp alisema anaelewa mvuto wa Kagawa kwa ligi ya Uingereza ambayo ni maarufu zaidi nchini Japan. Klopp ameliambia gazeti la Suddeutsche Zeitung kuwa hawawezi kuizuia ndoto ya Kagawa.
Man City mabingwa wa Uingereza
Bila shaka msimu wa kusisimua zaidi wa ligi ya soka Uingereza ulikamilika kwa mtindo wa aina yake jana Jumapili wakati Manchester City walipotwaa taji hilo baada ya kuwabwaga QPR magoli matatu kwa mawili. Hilo lilikuwa taji la kwanza la City baada ya miaka 44 lakini walishinda katika mazingira ya kushangaza wakati magoli yao Edib Dzeko na Sergio Aguero ya dakika za ziada yaliwapa ushindi wa 3 – 2 na kwuanyima Manchester United taji lao la 20.
Mchuano huo ulikuwa wa kusisimua na mashabiki wa City kujishika tama kwa kipindi kizima cha mchezo, baada ya kusikia kuwa United ilikuwa imeishinda Sunderland goli moja wka sifuri. Lakini City walidhihirisha umahiri wao katika dakika tano za ziada na kuhakikisha kuwa wanawanyamazisha mahasimu wao wa jiji la Manchester. City ilimaliza juu ya Ligi sawa na United kwa pointi 89, ijapokuwa na tofauti ya mabao manane. Huyu hapa mkufunzi wa City Roberto Mancini
Katika kuwapongeza mabingwa wapya wa Premier League Manchester City, Sir Alex Ferguson aliwakumbusha kuwa wana barabara ndefu ya kusafiri kabla ya kufikia kiwango sawa na Manchester United. Kando na msisimuko wa Manchester, klabu ya Bolton nayo ilivunjwa moyo baada ya kutoka sare ya magoli mawili kwa mawili na kujiunga na wenzao walioshushwa daraja pamoja na Wolverhamption Wanderers na Blackburn Rovers.
Kwingineko Arsenal na Tottenham walijikatia tiketi za kushiriki katika ligi ya mabingwa msimu ujao baada ya kumaliza katika nafasi ya nne bora. Arsenal iliishinda Westbromwich Albion magoli matatu kwa mawili huku nao Tottenham Hotspurs ikiishinda Fulham mabao mawili kwa sifuri. Newcastle ilimaliza katika nafasi ya tano baada ya kuzabwa na Everton magoli matatu kwa moja.
Lakini hata hivyo mkufunzi Harry Rednkapp na vijana wake wa Hotspurs watalazimika kusubiri kwa hamu matokeo ya fainali ya kombe la Ligi ya Mabingwa kati ya Bayern na Chelsea. Ushindi kwa Bayern utaipa fursa Spurs kushiriki katika dimba hilo msimu ujao, na ikiwa Chelsea itashinda basi itajikatia tiketi ya moja kwa moja na hivyo Spurs kuambulia patupu na kuridhika na ligi ya Ulaya yaani Europa League.
Biashara kuimarika Ukraine na Poland
Mashabiki wa soka wanakabiliwa na changamoto ya kuongezeka bei za vyumba vya kulala na hoteli pamoja na mikahawa na mabaa nchini Ukraine wakati wafanyabiashara wakijiandaa kupata faida katika kinyang'anyiro cha soka cha Euro 2012 ambacho kitaandaliwa kwa pamoja na Poland.
Rais wa shirikisho la soka Ulaya UEFA Michel Platini ameelezea shutuma kali kuhusu ongezeko la bei ambazo zimeripotiiwa kupanda mara kumi na akaitaka serikali ya Ukraine kuchukua hatua. Poland pia inaonyesha upande wake wa kibishara. Vyumba vya hoteli zilizo karibu na uwanja mpya uliojenga wa Warsaw vimepandishwa bei.
Na kwa kumalizia ni kuwa mshambulizi wa Malaga Ruud Van Nistelrooy leo amezitundika njumu zake kutoka soka ya kulipwa na kumaliza taaluma yake nzuri ya soka ambayo pia ilimpa nafasi ya kuzichezea Manchester United na Real Madrid. Mholanzi huyo mwenye umri wa miaka 35 amesema alicheza mchuano wake wa mwisho jana na sasa anahisi kuwa wakati umewadia kwake kuwacha kusakata soka kwa sababu mwili wake haurusuhu.
Mwandishi: Bruce Amani/AFP/Reuters/DPA
Mhariri: Othman Miraji