Dortmund walipiza kisasi kwa Bayern Münich
27 Aprili 2017Hii ni kufuatia kule kushindwa nyumbani kwao Allianz Arena katika nusu fainali ya kombe la Ujerumani na mahasimu wao Borussia Dortmund BVB usiku wa Jumatano.
Mabingwa hao wa Ujerumani walikuwa kifua mbele 2-1 kabla Dortmund kuwashangaza kwa kutoka nyuma na kutwaa ushindi wa 3-2. Haya yote yanakuja wiki moja tu baada ya hao the Bavarias, kubanduliwa kutoka kwenye ligi ya mabingwa barani Ulaya na Real Madrid.
Bayern lakini bado wanaweza kulishinda taji la ligi kuu ya Ujerumani, Bundesliga, kwa mara ya tano mfululizo na ndilo jambo lililomfanya Ancelotti kukataa kuzungumzia ufanisi wake msimu huu, kwa sababu bado kuna mechi nne za ligi zilizosalia na wamebakisha pointi tano waweze kutawazwa mabingwa.
Hakuna wasiwasi wa kuachishwa kazi Ancelotti
"Ni mapema sana kwa hilo," alisema Ancelotti. "Tunastahili kuweka mambo wazi katika ligi kuu sasa haraka iwezekanavyo."
Kwa sasa hakuna wasiwasi wa kuachishwa kazi kwa Ancelotti, ingawa hajapata ufanisi mkubwa katika msimu wake wa kwanza, akilinganishwa na mtangulizi wake Pep Guardiola aliyehamia Manchester City. Guardiola aliifikisha Bayern Munich katika nusu fainali ya ligi ya mabingwa Ulaya na akashinda Bundesliga na kombe la shirikisho la Ujerumani, DFB Pokal, katika msimu wake wa kwanza.
Javi Martinez na Mats Hummels walikuwa wamefunga magoli mawili katika kipindi cha kwanza na kulifuta lile la mapema lililowapa Dortmund uongozi na ambalo lilitiwa kimyani na Marco Reus.
Dortmund walizinduka kipindi cha pili na kupata ushindi
Lakini katika kipindi cha pili, BVB walizinduka kutoka kwenye kile kichapo cha 4-1 walichopewa na hao wapinzani wao hapo Allianz Arena wiki tatu zilizopita katika mechi ya ligi. Pierre-Emerick Aubameyang alifunga goli lake la 35 la msimu baada ya kuandaliwa na Ousmane Dembele, kabla chipukizi huyo kutoka Ufaransa, kufunga goli la tatu na la ushindi la Dortmund, dakika 16 kabla mechi kukamilika.
Nahodha wa Bayern Philip Lahm atakayestaafu msimu utakapofikia kikomo alisema, "Tumeshushwa mabega pakubwa, tulitaka kufika fainali. Tunapokuwa tunaongoza mechi, inastahili kuwa vigumu kutushinda."
Bayern wanaweza kushinda taji la Bundesliga, iwapo Leipzig watashindwa kuwalaza FC Ingolstadt wanaoshikilia nafasi ya 17 na ambao wanapambana wasishushwe daraja. Ingolstadt ilikuwa timu ya kwanza kuifunga Leipzig katika mkumbo wa kwanza wa ligi kuu ya Ujerumani msimu huu na kiungo wao Alfredo Morales ameuambia wavuti wa klabu hiyo kwamba, iwapo wanataka kuwafunga tena, ni sharti wajizatiti sana.
Mwandishi: Jacob Safari/AFP/DPAE
Mhariri: Josephat Charo