1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Dortmund yaangazia macho Ligi ya Mabingwa

6 Oktoba 2012

Klabu ya Borussia Dortmund imeshinda mataji mawili mfulululizo ya Bundesliga, lakini msimu huu siyo wanaopigiwa upatu kwa sababu mahasimu wake, Bayern Munich, wamekiimarisha kikosi.

https://p.dw.com/p/16Lf5
Borussia Dortmund's Marco Reus (2nd R) celebrates his goal against Manchester City with team mates during their Champions League Group D soccer match in Manchester October 3, 2012. REUTERS/Phil Noble (BRITAIN - Tags: SPORT SOCCER)
Champions League Manchester City Borussia DortmundPicha: Reuters

Hayo ni kwa mujibu wa Afisa Mkuu mtendaji wa Borussia Dortmund Hans-Joachim Watzke, ambaye ameongeza kuwa Dortmund pia inaangazia ligi ya Mabingwa. Dortmund wamepanda hadi katika nafasi ya tatu kwenye ligi baada ya mwanzo mbaya wa msimu. Na wametoka sare ya goli moja kwa moja na Manchester City katika mchuano wao wa kundi D wa Ligi ya Mabingwa wa Ulaya Jumatano iliyopita, huku wenyeji wakihitaji penalty katika dakika ya 90 ili kusawazisha.

Mwendo wao wa kasi dhidi ya mabingwa hao wa Uingereza uliwanyamazisha wahakiki nyumbani waliosema kwamba wao ni moto wa kuotea mbali tu katika ligi ya nyumbani. Watzke anasema mwaka jana hawakufanya viziri katika ligi ya mabingwa kwa sababu walihitaji ujuzi. Sasa msimu huu wako tayari kujaribu kuimarika.

Borussia Dortmund waliwakaba Manchester City kwao Uingereza
Borussia Dortmund waliwakaba Manchester City kwao UingerezaPicha: Reuters

Watzke alisaidia kubadilisha mambo baada ya kujiunga na klabu hiyo mnamo mwaka wa 2005, kuiokoa klabu ambayo ilikuwa imefilisika na kuifanya kuwa mojawapo ya vilabu vilivyofanikiwa zaidi Ujerumani katika misimu miwili iliyopita. Mahasimu wao, Bayern Munich, wako mbele na tofauti ya pointi saba baada ya kushinda mechi zao zote sita za kwanza.

Bayern ilitumia euro milioni 40 kumpata kiungo wa Uhispania Javi Martinez, na pia ikawasajili washambuliaji Mario Mandzukic na Claduio Pizarro pamoja na mchezaji wa kimataifa wa Uswisi, Xherdan Shaqiri. Dortmund wameshindwa tu mchuano mmoja katika mechi tisa kwenye vinyang'anyiro vyote, ikwia ni kichapo cha magoli matatu kwa mawili dhidi ya Hamburg SV mwishoni mwa mwezi Septemba ambao ulivunja rekodi yao ya kutoshindwa mechi 31 mfululizo katika ligi.

Mshambulizi wa zamani wa Ujerumani Magharibi, Dieter Mueller, yuko katika hali mahututi baada ya kupatwa na mshutuko wa moyo. Mojawapo ya vilabu vyake, Offenbach Kickers, ilitangaza jana, ijumaa.

Dieter MUELLER akiwa na ngao ya Bundesliga mnamo mwaka wa 1978
Dieter MUELLER akiwa na ngao ya Bundesliga mnamo mwaka wa 1978Picha: picture-alliance/Sven Simon

Mueller, mwenye umri wa mika 58, ambaye alifunga magoli matatu dhidi ya Yugoslavia katika nusu fainali ya Ubingwa wa Ulaya, mnamo mwaka wa 1976, alizirai nyumbani kwake na kusaidiwa na mkewe kurejesha fahamu, kabla ya kukimbizwa hospitalini. Mueller ni mmoja wa washambuliaji mashuhuri katika historia ya ligi ya Bundesliga, kwa kufunga magoli 159 katika mechi 248 alizoichezea klabu yake ya Cologne kwa miaka minane, na akawa mfungaji bora wa ligi ya Ujerumani katika msimu wa mwaka wa 1977 na 1978. Alifunga jumla ya idadi ya magoli 177 katika mechi 303 za Bundesliga huku akiwahi kuchezea Offenbach, VfB Stuttgart, na Saarbruecken. Magoli yake sita aliyoifungia Cologne katika mchuano waliopata ushindi wa magoli saba kwa mawili dhidi ya Werder Bremen mnamo tarehe 17 Agosti mwaka wa 1977 yanasalia kuwa rekodi ya Bundesliga hadi kufikia sasa.

Di Matteo awatetea wachezaji wa Chelsea

Meneja wa Chelsea, Roberto Di Matteo, amewatetea wachezaji wake baada ya Ashely Cole kuandika kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii, twitter, ujumbe wa matusi, muda mfupi baada ya Shirikisho la Soka Uingereza, FA, kutoa ripoti iliyoshutumu ushahidi wake katika kesi ya ubaguzi iliyomkabili John Terry.

Cole, mwenye umri wa miaka 31, aliijibu ripoti iliyoeleza ni kwanini FA ilimpiga mafuruku Terry kucheza mechi nne na kumtoza faini ya pauni 220,000 kwa kumtolea matamshi ya kibaguzi beki wa Queens Park Rangers, Anton Ferdinand. Di Matteo alisema kikosi chake kina nidhamu na kwamba anaweza tu kuamua kuhusu suala hilo kulingana na wanachofanya uwanjani.

Mwandishi: Bruce Amani/DPA/AFP/Reuters
Mhariri: Miraji Othman