Dortmund yaionya Bayern kabla ya fainali
17 Mei 2013Mkufunzi wa Borussia Dortmund Jurgen Klopp amesema ana matumaini kwamba timu yake inaweza kuizidi nguvu Bayern Munich na kumaliza safari yao ya kujiondoa kutoka maisha ya kufilisika iliyoanza mwaka wa 2005.
Dortmund watapambana na Bayern katika uwanja wa Wembley mnamo Mei 25 kwa ubingwa huo wa Ulaya, ikiwa ni miaka minane baada ya kuomba mkopo wa euro milioni mbili kutoka kwa mahasimu wao hao Bayern ili kuwalipa mishahara wachezaji.
Klopp anasema kama watashinda, hawatakuwa timu bora ulimwenguni, lakini watakuwa wameipiku timu bora ulimwenguni kwa sasa. Hata hivyo amekiri kuwa mabingwa hao wa msimu huu wa Bundesliga Bayern, wanastahili kupigiwa upatu katika kile kitakachokuwa ni Fainali ya kwanza kuwahi kuchezwa na vilabu viwili vya Ujerumani. Na bila shaka Kansela Angela Merkel amedhibitisha kuwa atahudhuria fainali hiyo katika uwanja wa Wembley ili kuwa sehemu ya historia. Ijapokuwa amekataa kuitaja timu atakayoishabikia kati ya hizo mbili.
Kocha Löw ataja kikosi cha Ujerumani bila wachezaji nyota
Kocha wa timu ya taifa ya Ujerumani Joachim Löw amewaita kikosini wachezaji wane wapya kwa mechi za kirafiki za Ujerumani dhidi ya Ecuador na Marekani, huku nyota wa Bayern Munich na Borussia Dortmund wakiwachwa nje kwa sababu ya fainali ya Champions League.
Wachezaji wa Real Madrid Mesut Oezil na Sami Khedira pia watakosa ziara hiyo kwa sababu msimu wa Ligi ya Uhispania hautakuwa umekamilika. Jumla ya wachezaji 15 wa kikosi cha kwanza hajawajumuishwa katika ziara hiyo ya Marekani. Ujerumani itamenyana na Ecuador Mei 29 mjini Boca Raton na kasha Marekani mnamo Juni 2 mjini Washington DC.
Mshambulizi wa Lazio Miroslav Klose na wachezaji wawili wa Borussia Dortmund, Kevin Grosskreutz and Sven Bender, wanatarajiwa kujiunga na kikosi cha taifa baada ya kumaliza majukumu ya klabu yao, kwa mechi ya kirafiki dhidi ya Marekani. Wachezaji wapya walioitwa kikosini ni beki Philipp Wollscheid wa Nuremberg, viungo Sidney Sam wa Bayer Leverkusen, Nicolai Mueller wa Mainz na Max Kruse wa Freiburg. Wengine walioitwa ni viungo Aaron Hunt (Werder Bremen) na Stefan Reinartz (Bayer Leverkusen).pamoja na mabeki Dennis Aogo (Hamburger SV) na Andreas Beck (Hoffenheim).
Beckham azitundika njumu
Wiki mbili zilizopita kumeshuhudiwa maamuzi ya kustaafu kutoka kwa wachezaji kadhaa wa kabumbu nchini Uingereza, na jina la hivi punde kuongeza kwenye orodha hiyo ni David Beckham. Nahodha huyo wa zamani wa Soka ya Uingereza ameamua kustaafu kutoka soka mwisho wa msimu huu.
Beckham mwenye umri wa miaka 38 alijiunga na timu ya Paris St-Germain ya Ufaransa mapema mwezi wa Januari kwa kandarasi fupi ya miezi mitano. Wakati wa kutia saini kandarasi hiyo nyota huyo wa kabumbu alitangaza kwamba mshahara wake wote atautoa kwa mashirika ya kutoa msaada.
Beckham alijunga na timu ya Manchester United akiwa na umri wa miaka 14 na kufaulu kuichezea klabu hiyo mechi 398 huku akishinda mataji sita ya Premier League na kombe la klabu bingwa barani Ulaya. Nyota huyo Muingereza amesema kuwa anaishukuru sana timu ya PSG kwa kumpa fursa ya kuendelea kucheza lakini anahisi kuwa huu ni wakati mzuri kwake kumaliza kazi yake ya kucheza mpira. Pamoja na PSG kubeba kombe la Ligue 1 la Ufaransa, katika uchezaji wake Beckham amezoa jumla ya mataji 19 - 10 kati yao yakiwa ni mataji ya ligi kuu mbali mbali ulimwenguni. Bechkam ndie mchezaji wa kwanza wa Uingereza kuwahi kubeba makombe ya ubingwa wa Ulaya akichezea timu katika nchi nne tofauti.
Mwandishi: Bruce Amani/DPA/AFP
Mhariri: Yusuf Saumu