DRC imeahirisha chanjo dhidi ya Covid-19
15 Machi 2021Operesheni ya kutoa chanjo hiyo ilikuwa imepangwa kuanza leo Jumatatu, lakini kulingana na taarifa ya Wizara ya Afya ya nchini jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo,zoezi hilo litafanyika tu baada ya uchunguzi juu ya athari za chanjo ya Astra Zeneca kukamilika.
Ni zaidi ya wiki moja tangu Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kupokea dozi zaidi ya milioni moja na laki Saba na hivyo kuwa moja ya nchi za kwanza barani Afrika kupokea chanjo hizo zilizoidhinishwa na kusafirishwa chini ya mpango wa COVAX. Lakini kwa tahadhari, viongozi wa Kongo wameamua kuahirisha uanzishaji wa kampeni ya chanjo hiyo, kama ilivyofanywa na baadhi ya nchi za Ulaya kutokana na ripoti kwamba watu waliopewa chanjo hizo wanapata matatizo ya kuganda damu.
Zoezi la chanjo linasubiriwa kwa hamu kubwa mjini Kinshasa
Mjini Kinshasa unasubiriwa uthibitisho kutokana na madai hayo, kama anavyoeleza Daktari Eteni Longondo, Waziri wa Afya wa Kongo, ambaye anasisitiza umuhimu wa chanjo hiyo anasema "Chanjo ndio njia bora zaidi kwa kumaliza janga. Tunasubiri kuhitimishwa kwa utafiti unaoendeshwa na Wazungu, pia ule wa kamati yetu ya kisayansi hapa nyumbani ili kuchukuwa hatua ya mwisho. Ila kwa sasa, tumesitisha," alisema waziri huyo.
Hatua hiyo ya serikali ya Kongo imechukuliwa baada ya mbunge Bertin Mubonzi kutoka chama cha UNC kumuuliza Waziri wa afya swali la usalama wa chanjo hiyo. Bertin Mubonzi sasa ameridhishwa na hatua hiyo, akisisitiza kwamba ni faida ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kuzingatia kinachoendelea katika nchi nyingine, ili kuwakinga raia wa Kongo.
Zaidi anasema "Tunaipokea vizuri hatua iliyochukuliwa na mamlaka ili kusimamisha operesheni. Kwa wazi tukizingatia ukweli huo, nadhani wakati itafafanuliwa yaani kuwahakikishia raia, bila shaka chanjo hiyo itapokelewa." Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo inayo mikoa 26 na miongoni mwa mikoa hiyo, ni 23 ndiyo kwa sasa imeathiriwa na covid-19.
Chanzo: DW Kinshasa