DRC: Juhudi za kusaka utulivu wa Kivu Kaskazini zaendelea
3 Agosti 2020Jimbo hilo limekumbwa na misukosuko ya ukosefu wa usalama kwa zaidi ya miongo miwili. Raia wake wamekuwa wakiishi katika hali ya vurugu kutokana na kuongezeka kwa idadi ya makundi ya waasi wanaovichoma vijiji moto.
Katika hotuba yake ya ufunguzi wa kikao hicho kilichodumu kwa siku tatu mfululizo jijini Goma gavana wa mkoa huo Carly Nzanzu Kasivita alibaini kuwa hiyo itakua njia mbadala ya kudumisha usalama wa wakaazi
Wakati huohuo wawakilishi wa mashirika ya kiraia wamedai kuwa bado mkoa huo utaendelea kukabiliwa na uvamizi mkubwa wa makundi ya wanamgambo kutoka nje na ndani ya Congo kufuatia kile walichokiita uzembe wa serikali kushindwa kugunduwa chanzo kinachowapelekea mamia ya vijana kujiunga na makundi hayo ya waasi na kusababisha wasiwasi mkubwa kwa raia.
Akizungumza na vyombo vya habari Thomas D'aquin Muiti ambaye ni msemaji wa mashirika ya kiraia nchini Congo amesema kikao hicho hakitoshi kumaliza tofauti kati ya makabila yanayo zozana mashariki mwa Congo kila uchao.
Haya yanajiri siku chache tu baada ya wawakilishi wa asasi za kiraia mkoani Kivu ya kaskazini kutangaza kurudi upya kwa kundi la waasi wa M23 ambao wameanzisha harakati zao wilayani Rutshuru. Hata hivyo tangazo hilo limeendelea kukanushwa na viongozi wa kundi hilo lililowahi kuuteka mji wa Goma mnamo Novemba 2012.