DRC yafufua migodi iliyokufa
24 Oktoba 2007Wakiishi katika eneo lenye mashimo na uharibifu mkubwa wa mazingira uliotokana na machimbo ya madini ya shaba, wakazi wa eneo la Kolwezi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo-DRC, wanaweza kupata neema upya kutokana na kuzungukwa na maliasili hiyo ambayo itaanza kuchimbwa tena.
Mgodi wa Kolwezi ulioko Kusini Mashariki mwa DRC ulilazimika kufungwa miongo miwili iliyopita, wakati wa utawala wa Rais Mobutu Sese Seko aliyetuhumiwa kwa kupora mali na rasilimali nyingi za nchi hiyo, iliyokuwa ikijulikana kwa jina la Zaire hapo zamani.
Ofisa mmoja wa masuala ya madini kutoka kampuni moja ya Canada iliyowekeza katika sekta ya madini huko Katanga katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Martin Christie amesema kwa kipindi cha miaka michache mabadiliko makubwa yamefikiwa zikiwa ni harakati za kufufua mgodi wa Kolwezi unaosemekana kuwa mkubwa duniani.
Baada ya kufungwa wakati wa utawala wa Rais Mobutu Sese Seko aliyekuwa akihusishwa na vitendo vya kidikteta, mgodi huo ulibakia kuwa bohari ya vyuma chakavu baada ya mitambo iliyokuwa ikitumika kuharibika kutokana na kutu pamoja na kuchakaa kwa ujumla.
Kutokana na eneo hilo kutokuwa na manufaa yoyote kwa serikali, lilitengwa kiasi kwamba hata huduma za kijamii hazikuwepo kwa ajili ya watu waliokuwepo.
Baada ya serikali ya DRC kuzinduka, sasa eneo hilo limekuwa na kituo cha kujaza mafuta kwa ajili ya magari, pamoja na miundombinu muhimu ikiwemo barabara ili kuwezesha mawasiliano, baada ya kipindi kirefu cha wananchi kutaabika.
Kuwepo na maendeleo hayo katika ufufuaji wa mgodi wa shaba wa Kolwezi huko Kusini Mashariki mwa DRC, mamia ya watu wameanza kupata faida ikiwemo ajira kwa wananchi ambao hapo awali, walikuwa wachimbaji wadogo tena haramu, huku wengine wakiajiriwa katika ofisi za utumishi na kijamii.
Kutokana na hali ya kisiasa nchini DRC kuanza kuwa ya kuridhisha tangu kutokea mgogoro mkubwa wa kisiasa na vita ya kiraia kuanzia mwaka 1998 hadi 2003, makampuni mengi ya kigeni yameonesha shauku ya kutaka kuwekeza katika sekta ya madini nchini humo.
Hadi sasa ni makampuni ya BHP Billiton na Anglo American yaliyoanza kujongea kwenye maeneo yenye utajiri wa madini katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo baada ya kufanyika uchaguzi wa kwanza wa kidemokrasia katika kipindi cha miaka 40 hapo mwaka jana.
Moja ya mgodi unaofanyiwa ukarabati uko kilometa kumi na mbili nje kidogo ya mji wa Kolwezi ambao hapo awali ulikuwa na kiasi kikubwa cha wachimbaji haramu, hivyo kutoinufaisha serikali wala watu wanaoishi katika maeneo hayo.
Mmoja wa wachimbaji wadogo Bwana Tshegeka Nwegi, amesema shughuli ya uchimbaji ilikuwa ngumu kwa wakati huo na kwamba amekuwa akiifanya kwa kipindi cha miaka saba, kwa vile hakuwa na jinsi nyingine ya kujikimu, ikizingatiwa kwamba ana familia za kutunza na watoto wanne wa kusomesha.
Baada ya kipindi kirefu cha mahangaiko sasa Bwana Tshegeka anafanya kazi katika mgodi wa Katanga akiwa mmoja wa maofisa wa miradi ya maendeleo kutokana na uzoefu wake.
Hata hivyo takwimu zinaonesha kwamba zaidi ya watu elfu 25 bado wanajishughulisha na uchimbaji haramu katika mgodi wa Kolwezi, na wengine zaidi ya elfu kumi wakifanya shughuli kama hiyo kwenye mgodi wa Katanga wenye kilometa za mraba 157.