1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

DRC yajadili hoja ya kutowashitaki marais wastaafu

Sylvia Mwehozi
22 Juni 2018

Pendekezo la sheria ya kinga ya kutoshitakiwa marais wa zamani nchini Kongo limeanza kujadiliwa kwenye baraza la seneti mjini Kinshasa, ikielezwa kuwa ni njia ya rais Joseph Kabila kuondoka madarakani.

https://p.dw.com/p/306LF
Angola | Ankunft des kongolesischen Präsidenten Joseph Kabila bei einem meeting der süd- und zentralafrikanischen Staaten in Angola
Picha: REUTERS/K. Katombe

Hata hivyo, upinzani umesema bado sheria hiyo ni lazima kutowahusisha viongozi wa taasisi zingine ambazo wengi wao wamehusika na ukiukaji wa haki za binadamu. Pendekezo hilo la sheria limeanza kusomwa upya miaka mitatu baada ya Seneta Modeste Mutinga kulipendekeza kwenye baraza la seneti kufuatia kile alicholelezea kuwa ni kinga ya kisheria kwa marais wa zamani mara watakapoachia madaraka.

Katiba ya Kongo inaelezea kwamba rais wa zamani ambaye alichaguliwa kidemokrasia anabaki kuwa seneta mnamo kipindi cha maisha yake yote. Lakini Rais Kabila aliamuru wiki iliyopita kwamba kuweko na sheria mpya kuhusu kinga kwa marais wa zamani. Tume maalumu ya seneti iliyoundwa kwa ajili ya kuchunguza kwa kina pendekezo hilo, inaelezea kwamba ikulu ya rais Joseph Kabila ilipendekeza kwamba kinga hiyo iwahusishe pia viongozi wa taasisi na idara kadhaa za kitaifa, hususan maspika wa bunge na seneti, wakuu wa jeshi na polisi na wale wa idara za upelelezi na uhamiaji.

Demokratische Republik Kongo Wahlmaschine
Vifaa vya uchaguzi nchini DRC vitakavyotumika uchaguzi wa mwaka huuPicha: Getty Images/AFP/J. Wessels

Upinzani umetupilia mbali pendekezo hilo na kusema ukimuacha rais, kila mtu ni lazima aweze kujibu kwa makosa aliyoyafanya ikiwa kuna vitendo vya rushwa na uhalifu. Sheria hiyo inapendekeza kwamba rais wa zamani ambaye alichaguliwa kidemokrasia mara ynapostaafu anapewa ulinzi wake binafsi na familia yake, na bajeti ambayo itamruhusu kuishi maisha mazuri, ikiwemo kupewa makaazi. Na ikiwa amefariki, mkewe na watoto wa chini ya umri wa miaka 18 wataendelea kufaidika na fedha hizo. Gregoire Lusenge, mbunge wa kutoka jimbo la Haut-Uele amesema kwamba kuweko na sheria hiyo kutawapa imani viongozi walioko madarakani kuhusu mustakbali wao na familia zao.

Kikao hiki maalumu cha bunge kilipendekezwa na Rais Joseph Kabila ambaye anatarajiwa kuhutubia taifa kuhusu hali ya kisiasa na kiusalama nchini. Baada ya kusomwa kwenye baraza la seneti pendekezo hilo la sheria litasomwa pia bungeni kabla ya kuidhinishwa na Rais Kabila.

Kongo Protest & Ausschreitungen gegen Präsident Joseph Kabila in Kinshasa
Vijana wakishiriki katika maandamano ya kumpinga rais Joseph KabilaPicha: picture-alliance/AP Photo/J. Bompengo

Wadadisi wa maswala ya kisiasa wanaelezea kwamba kuidhinishwa kwa sheria hiyo ni ishara kwamba Rais Kabila hatowania muhula wa tatu kama wanavyoelezea wapinzani. Hivi sasa mjadala ni kuhusu matumizi ya mfumo wa kieletroniki wakati wa uchaguzi, ambapo tume huru ya uchaguzi imetangaza kupokea shehena ya  kompyuta 1,200 miongoni mwa laki moja zinazosubiriwa ifikapo Septemba mwaka huu.

Naibu mwenyekiti wa CENI, Norbert Basengezi, amesema kwamba kompyuta hizo zitasambazwa kila mahala kabla ya uchaguzi na kila mpigaji kura anatakiwa kujaribu kompyuta hiyo kabla ya Desemba 23. Upinzani na mashirika ya kiraia wanaelezea wasiwasi wao kuhusu matumizi ya kompyuta hizo ambazo wanasema huenda yakachangia wizi wa kura kwa manufaa ya chama tawala. Madai ambayo yanatupilia mbali na tume ya uchaguzi, CENI.

Mwandishi: Saleh Mwanamilongo/DW Kinshasa
Mhariri: Mohammed Khelef