1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

DRC yatakiwa kuondoa marufuku dhidi ya maandamano

Caro Robi
22 Mei 2018

Baraza la Usalama la UN limeitaka DRC kuondoa marufuku iliyotangazwa Septemba 2016 dhidi ya maandamano kabla ya uchaguzi mkuu baadaye mwaka huu

https://p.dw.com/p/2y6Jk
Demokratische Republik Kongo Proteste gegen Kabila
Picha: Reuters/T. Mukoya

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, limeitaka serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo kuondoa amri inayopiga marufuku maandamano, kabla ya uchaguzi mkuu muhimu unaokusudiwa kumaliza utawala wa rais Joseph kabila. Baraza hilo lilikutana  katika kikao cha faragha kufuatia ombi la Ufaransa, kusikiliza ripoti ya mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa Leila Zerrougui (ZERUGI), kuhusu maandalizi ya  uchaguzi wa Desemba 23, utakaoweza kufungua njia ya kukabidhiana madaraka kwa mara ya kwanza katika taifa hilo lenye utajiri wa mali asili.

Balozi wa Poland Joanna Wronenka anayeshikilia Uenyekiti wa Baraza la usalama kwa mwezi huu, aliwaambia waandishi habari baada ya mkutano wao, kwamba Baraza hilo limewataka maafisa nchini Congo kuondoa vikwazo vya kisiasa  na kuondoa amri inayopiga marufuku maandamano. Amri hiyo ilitangazwa  Septemba 2016, zilipozuka fujo wakati wa maandamano ya kumpinga Rais Kabila.