Droo ya hatua ya mchujo Ligi ya Mabingwa Ulaya
11 Desemba 2017Mabingwa watetezi Real Madrid wamepangwa kukutana na Paris Siant Germain katika hatua ya 16 za mwisho ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Chelsea watakutana na Barcelona wakati makamu bingwa wa msimu uliopita Juventus wataangushana na Tottenham Hotspur. Roma watakwaruzana na Shakhtar Donetsk. Basel watakuwa wenyeji wa Manchester City, Porto itaangushana na Liverpool nao Sevilla watacheza na Manchester United. Mabingwa mara tano Bayern Munich pia wanatabasamu baada ya kupangwa na Besiktas.
Mechi za mkondo wa kwanza zitachezwa Februari 12/14 na Februari 20/21, za marudiano itakuwa Machi 6/7 na 13/14. Fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya itafanyika Kiev mnamo Mei 26.
Kwingineko, Real Madrid wako katika nchi ya Umoja wa Falme za Kiarabu wakilenga kuweka historia ya kuwa timu ya kwanza kuhifadhi Kombe la Klabu Bingwa duniani na kuwa kwenye kundi moja na mahasimu wao Barcelona kwa kushinda mataji matatu. Real watacheza dhidi ya Al Jazira siku ya Jumatano mjini Abu Dhabi kabla ya kucheza katika fainali au mechi ya mshindi wa tatu siku ya Jumamosi. Gremio ya Brazil, mabingwa wa mwaka wa 2017 wa Copa Libertadores, au Pachuca ya Mexico, mabingwa ligi ya mabingwa ya CONCACAF watakuwa na hamu ya kukutana Madrid, mabingwa wa kombe la klabu bingwa duniani wa mwaka wa 2014 na 2016.
Mwandishi: Bruce Amani/AFP/AP/DPA/Reuters
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman