El-Sisi kuwa mwenyekiti wa AU
10 Februari 2019Kipindi cha Misri cha uongozi "huenda kikaelekezwa katika usalama na ulinzi wa amani", amesema Ashraf Swelam, ambae anaongoza taasisi ya uchunguzi wa masuala ya kisiasa yenye uhusiano na wizara ya mambo ya kigeni ya nchi hiyo.
Mwenyekiti wa AU anayeingia madarakani rais Abdel Fattah al-Sisi anaonekana kuelekea kutolenga "mageuzi ya masuala ya fedha na utawala" kama ilivyokuwa kwa mtangulizi wake , Swelam aliongeza.
Mageuzi ya aina hiyo yalikuwa alama muhimu ya mwenyekiti wa AU anayeondoka madarakani Paul Kagame . Rais huyo wa Rwanda amekuwa akisukuma kuundwa kwa mfuko wa kodi ya mauzo ya biadhaa zinazoingizwa katika bara hilo kutoka nje na kupunguza utegemezi wa bara hilo kwa wafadhili wa nje, ambao bado wanalipa fedha kwa ajili ya nusu ya bajeti ya taasisi hiyo kila mwaka.
Mataifa makubwa ya Afrika
Mwanadiplomasia wa Afrika aliliambia shirika la habari la AFP kwamba Misri , pamoja na mataifa mengine yenye uchumi mkubwa Afrika kusini na Nigeria hazitaki AU yenye nguvu.
Mwanadiplomasia huyo, ambaye amekuwa akifuatilia masuala ya AU kwa muda wa muongo mmoja, amesema Misri "Haijasahau" kusitishwa kwake uanachama mwaka 2013.
Kuwekwa kando kwa karibu mwaka kutoka katika Umoja wa Afrika kulikuja baada ya jeshi la Misri kumuondoa madarakani rais Mohamed Mursi, ambaye mwaka 2012 alikuwa rais wa kwanza nchini humo aliyechaguliwa kidemokrasia.
Sisi anatarajiwea kuchukua hatamu za kuuongoza Umoja wa Afrika katika baraza la mataifa hayo la miaka miwili, ambalo lianza kikao chake Februari 10 na 11 katika makao makuu ya Umoja huo katika mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa.
Kama kawaida, mizozo kadhaa ya bara hiyo ya kiusalama itakuwa juu katika ajenda ya viongozi hao. Pendekezo la Rwanda la kupata mfuko wa kugharamia bajeti ya bara hilo pia itakuwa sehemu ya majadiliano.
Lakini pendekezo hilo limekumbana na upinzani sio tu kutoka Misri, lakini mataifa mengi wanachama, kwa hiyo inawezekana kuwa halitapita.
Mageuzi katika AU
Mageuzi ya halmashauri ya AU ni mada nyingine nyeti zaidi. Novemba mwaka 2018, mataifa mengi yalikataa pendekezo la kutoa kwa chombo hicho cha utendaji cha AU, madaraka ya kuwateua wabunge pamoja na makamishina.
Lakini Misri "wako tayari" katika kusukuma mageuzi mengine ya AU, kwa mujibu wa afisa mmoja wa Umoja huo.
Juhudi moja muhimu inayoungwa mkono na Cairo ni eneo la biashara huru la bara hilo CFTA, juhudi zilizokubalika na mataifa 44 kati ya 55 wanachama mwezi Machi 2018.
Soko la pamoja ni nguzo ya mpango wa Umoja wa Afrika wa "Ajenda 2063", uliotayarishwa kama mfumo wa mkakati kwa ajili ya mabadiliko ya uchumi wa jamii.
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe
Mhariri: Grace Patricia Kabogo