Ethiopia, Eritrea zafungua tena mpaka wao baada ya miaka 20
11 Septemba 2018Vikosi vya majeshi ya Ethiopia na Eritrea vilivyowekwa kwenye maeneo ya mpakani vitaondolewa na kurejeshwa aktika kambi ili kutuliza wasiwasi, alisema waziri mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed.
"Tunaukaribisha mwaka mpya kwa kuvunja mahandaki yalioko mpakani mwetu," Abiya aliwaambia waandishi habari, akimaanisha ukweli kwamba mwaka mpya wa Ethiopia ulisherehekewa siku ya Jumanne.
"Kuanzia leo, vikosi vya ulinzi vya Ethiopia (kwenye mpaka na Eritrea) vitakusanywa katika kambi na kupunguza wasiwasi uliokuwa mkubwa mara nyingi. Hatua kama hiyo itachukuliwa pia upande wa Eritrea.
Maelfu ya watu kutoka mataifa yote mawili walifuatilia hafla ya ufunguzi wa vituo hivyo vya mpakani mjini Zalambessa, ambao ni mji wa mpakani wa Ethiopia ulioangamizwa mara baada ya kuzuka uhasama kati ya majirani hao mnamo mwaka 1998.
Wanajeshi wa raia wakipeperusha bendera za Ethiopia na Eritrea walijipanga barabarani wakati waziri mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed na rais wa Eritrea Isaias Afwerki walipofungua mpaka katika sherehe iliotangazwa moja kwa moja kupitia televisheni ya taifa ya Ethiopia.
"Hii ndiyo siku ya furaha zaidi katika maisha," alisema Ruta Haddis, raia wa Eritrea kutoka mji wa Senafe, umbali mfupi tu kutoka mpakani. "Sikufikiria kama siku hii ingetokea katika maisha yangu."
Mwanzo wa uhasama baina ya majirani hao
Vita vya kuwania mpaka na masuala mengine vilisababisha vifo vya watu takribani 80,000 kabla ya kumalizika kwa mapigano mwaka 2000 kufuatia makubaliano ya amani yaliobishaniwa.
Hali ya wasiwasi iliendelea kushuhudiwa kuhusiana na eneo la mpaka - hadi pale Abiy alipojitolea kumaliza mkwamo huo wa kijeshi mwaka huu kama sehemu ya mageuzi aliokuja nayo, ambayo yamebadili mandhari ya kisiasa katika eneo la pembe ya Afrika na zaidi.
Viongozi hao wawili pia walifungua kivuko kingine katika mpaka wa Bure, alisema waziri wa mawasiliano wa Ethiopia Yemane Meskel katika ujumbe wa twitter. Kivuko cha Debay Sima - Bure kinaelekea kwenye bandari ya Assab mashariki mwa Eritrea, wakati badari yake ya Massawa inapatikana moja kwa moja kaskazini kwa barabara ya Serha - Zalambessa.
Ethiopia, taifa linaloinukia kiuchumi la wakaazi milioni 100, lilikuwa linaitegemea Djibouti kwa karibu asilimia 100 kwa usafirishaji kwenda na kutoka bahari ya Sham tangu mwaka 1998.
Mwaka mpya wa Ethiopia
Picha zilizowekwa mtandaoni na mkuu wa shughuli za ofisi ya Abiy ziliwaonyesha viongozi hao wakitembea sambamba mjini Bure - Abiy akiwa katika sare za kijeshi na Isaias akivalia malapa na kaunda suti. Eneo la Bure lilishuhudia mojawapo ya mapigano makali zaidi wakati wa vita vya 1998-2000.
Viongozi hao wa Eritrea na Ethiopia wamechukuwa hatua za haraka kukomesha uhasama uliodumu kwa miongo miwili tangu waliposaini makubaliano ya mjini Asmara hapo Julai 9 kurejesha uhusiano baina mataifa yao.
Eritrea ilifungua tena ubalozi wake nchini Ethiopia mwezi Julai, na Ethiopia ikachukuwa hatua kama hiyo wiki iliyopita na mataifa hayo yamerejesha pia safari za ndege baina yao.
Viongozi hao wawili waliadhimisha mwaka mpya wa Ethiopia pamoja kwenye mpaka, pamoja na majeshi yao siku ya Jumanne, alisema mkuu wa shughuli ya Abiy, Fitsum Arega.
Ethiopia inafuta kalenda inayofanana na kalenda ya kale ya julian - ambayo ilianz kutoweka katika mataifa ya magahribi katika karne ya 16 - hii ikimaanisha kuwa nchi hiyo ilingia mwaka wake wa 2011 siku ya Jumanne.
Mwandishi: Iddi Ssessanga/rtre.
Mhariri: Lillian Mtono