1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Ulaya waidhinisha fedha kushughulikia wahamiaji

11 Agosti 2015

Umoja wa Ulaya umeidhinisha fungu la euro bilioni 2.4 ambalo litatumiwa kuzisaidia nchi kama Italia na Ugiriki ambazo zinapokea idadi kubwa ya wahamiaji wanaoingia barani Ulaya.

https://p.dw.com/p/1GD72
Idadi kubwa ya wakimbizi wanaoingia Ulaya imesababisha mgogoro
Idadi kubwa ya wakimbizi wanaoingia Ulaya imesababisha mgogoroPicha: picture alliance/ROPI

Halmashauri Kuu ya Ulaya ilitangaza jana jioni kuwa kati ya fedha hizo zilizoidhinishwa, Italia itapokea kiasi cha euro milioni 558, huku Ugiriki ikipata euro milioni 478. Bajeti hiyo ni ya kipindi cha miaka sita, kushughulikia idadi kubwa ya wahamiaji wanaoingia barani Ulaya, wengi wakipitia mipaka ya nchi hizo mbili.

Fedha hizo zitaziwezesha nchi zitakazozipokea kuchunga mipaka na kuimarisha mpango wa kuwarudisha nyumbani kwao wale ambao maombi yao ya hifadhi yatakataliwa. Msemaji wa Halmashauri Kuu ya Ulaya Natasha Bertaud amesema fedha hizo zipo tayari kukabidhiwa kwa nchi zinazohusika, na kuongeza kuwa Ulaya inauchukulia mzozo wa wahamiaji kwa umakini mkubwa.

''Tumetangaza leo kutolewa kwa euro bilioni 2.4 kuzisaidia nchi wanachama kukabiliana na shinikizo la wahamiaji, na Halmashauri Kuu ya Ulaya itaendelea kufanya iwezavyo kushirikiana na nchi wanachama kuishughulikia changamoto hiyo''. Amesema Bertaud.

Mzozo wa Calais pia wazingatiwa

Mbali na Italia na Ugiriki, Uhispania pia itapokea kiasi cha euro milioni 521.8, Sweden itapata euro milioni 154, na Cyprus imetengewa euro milioni 74.

Hali kadhalika, awali Uingereza na Ufaransa zinazokumbwa na mzozo wa wakimbizi katika eneo la Calais lililo karibu na njia ya chini ya bahari, zilipatiwa fedha za dharura kushughulikia mzozo huo. Uingereza tayari imepokea euro milioni 27, nayo Ufaransa itapata euro milioni 20 mwishoni mwa mwezi huu. Hata hivyo fedha hizo siyo sehemu ya msaada ambao umetangazwa jana.

Úingereza na Ufaransa zinakabiliwa na mzozo wa pekee wa wahamiaji katika eneo la Calais
Úingereza na Ufaransa zinakabiliwa na mzozo wa pekee wa wahamiaji katika eneo la CalaisPicha: Reuters/P. Rossignol

Ugiriki na Italia zilizo kusini mwa Ulaya zimekuwa zikilalamikia idadi kubwa ya wakimbizi na wahamiaji inayoingia kupitia mipaka ya nchi hizo, zikisema miundo mbinu iliyopo haitoshelezi kukidhi mahitaji yao.

Hali ya kuaibisha

Ijumaa iliyopita, Umoja wa Mataifa ulitoa tahadhari, ukionya juu ya hali ya wakimbizi nchini Ugiriki, ambayo ulisema ni ya kuaibisha. Waziri Mkuu wa Ugiriki Alexis Tsipras alisema kuwa serikali yake isingeweza kumudu gharama za kuwatunza wahamiaji waliofurika kwenye kisiwa chake cha Aagean.

Wakimbizi wengi huwasili wakiwa na mahitaji makubwa ya msaada
Wakimbizi wengi huwasili wakiwa na mahitaji makubwa ya msaadaPicha: Getty Images/AFP/D. Dilkoff

Ugiriki itakabidhiwa sehemu ya kwanza ya msaada huo, kiasi cha euro milioni 33, mara tu itakapomaliza kuunda taasisi ya kuzishughulikia fedha hizo.

Nchi nyingine wanachama wa Umoja wa Ulaya ambazo zitanufaika na fungu hilo ni Hungary ambayo imepata euro milioni 61.4, Bulgaria itakayokabidhiwa euro milioni 72.7, na Romania ambayo itapewa euro milioni 98.3.

Poland kwa upande wake imepata euro milioni 69.3, nchi ya kisiwa ya Malta imetengewa euro milioni 74.6 nayo Ureno itasaidiwa kwa kiasi cha euro 38.6.

Kwa mujibu wa takwimu za umoja huo, wakimbizi takribani 124,000 wameingia barani Ulaya mwaka huu, hilo likiwa ongezeko la asilimia 750 ikilinganishwa na idadi ya wakati kama huu mwaka uliopita.

Mwandishi: Daniel Gakuba/afpe/rtre

Mhariri: Caro Robi