Gigaba kutetea sera za chama cha ANC
1 Aprili 2017Gigaba alichukuwa nafasi ya Pravin Gordhan aliyeondolewa katika wadhifa huo katika mabadiliko ya baraza la mawaziri ya ghafla usiku wa manane yaliyofanywa na Rais Jacob Zuma ambayo yameonyesha kuwepo mgawanyiko ndani ya chama hicho cha ANC.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Pretoria hapo Jumamosi (01.04.2017) Gigaba amesema "nitalenga sana katika kutekeleza sera za ANC katika kuboresha maisha ya Waafrika kusini walio wengi."
Hapo mwaka 2014 chama hicho cha ANC kilipitisha ya sera za mageuzi makubwa ya kiuchumi katika juhudi za kuharakisha kushirikishwa katika shughuli kuu za kiuchumi wananchi wa Kiafrika walio wengi ambao huko nyuma walikuwa wametengwa.
Amesema kumezidi kuwepo na maafikiano ndani ya chama hicho tawala kwamba kasi na ukubwa wa mageuzi hayo imekuwa ya taratibu mno na mara nyingi imekuwa haiendani na uhalisia.
Hana tajiriba ya kiuchumi
Hata hivyo kuchaguliwa kwa Gigaba kumezusha wasi wasi miongoni mwa vyama vya upinzani na waanangalizi wa masuala ya kiuchumi kutokana na kwamba hana misingi ya masuala ya fedha na kwa kiasi kikubwa anaonekana kama ni mshirika wa Rais Zuma.
Gigaba pia amesema kwamba anajuwa kwamba kuna tazizo la kutokuwepo na imani na serikali kwa hiyo ameahidi kuwatowatelekeza wananchi kwa kuruhusu maslahi ya watu maalum kudhuru wananchi.Amesema dhima yake ni "kurudisha utulivu" . Waziri huyo wa zamani wa mambo ya ndani na mkuu wa jumuiya ya vijana ya ANC hana tajiriba kubwa ya kiuchumi lakini amekubali kukutana na Gordhan.
Sarafu ya randi ya nchi hiyo mojawapo ya mataifa yenye nguvu kubwa za kiuchumi barani Afrika imeshuka thamani kutokana na wasi wasi wa kuwepo kwa rushwa katika ngazi ya juu serikalini.
Waziri huyo mpya amesema amejitolea kushikilia nchi hiyo kuwa katika kiwango inachostahiki kupewa mikopo ya uwekezaji na kwamba amekuwa akizungumza na mashirika yenye kupima uwezo wa nchi kulipa mikopo yake.
Amesema anafahamu fika juu ya mazingira yalioko sasa ya kugawika kwa nchi hiyo na kuchochewa kisiasa na ameahidi kutoyumbishwa na masuala ya nje.
Pigo kuondolewa kwa Gordhan
Kutimuliwa kwa Gordhan na naibu wake Mocebisi Jonas kumeelezewa na wakosoaji kuwa ni hatua iliyochukuliwa na Zuma kuwaweka wafuasi wake katika hazina.
Gordhan ambaye alikuwa akitetea utawala safi na alikuwa akiheshimiwa kimataifa kutimuliwa kwake kumezusha miito ya kumtaka Zuma ajiuzulu.Kuondolewa kwake wizara ya fedha ambako alikuwa ngome dhidi ya watu wanaotaka kuchota fedha hazina kwa maslahi binafsi ni pigo jengine kwa uchumi wa Afrika Kusini ambao ulikuwa tu kwa asilimia 0.5 mwaka jana ina ina kiwango cha ukosefu wa ajira cha asilimia 27.
Kuondolewa kwa mawaziri 10 katika mabadiliko ya baraza la mawaziri lenye mawaziri 35 kumezidisha fadhaa nchini Afrika Kusini ambapo fahari yake iko katika sifa zake za kidemokrasia zilizoundwa wakati wa mapambano dhidi ya utawala wa ubaguzi wa rangi na ambazo zimefifia kwa miaka sasa kutokana na kashfa zinazomzunguka Zuma.
Makamo wa rais Cyril Ramaphosa amekosowa kutimuliwa kwa Gordhan katika kauli ya nadra hadharani kumlaumu rais.
Mwandishi : Mohamed Dahman/AP
Mhariri : Lilian Mtono