Meloni asema Urusi ni tishio kwa usalama wa Umoja wa Ulaya
22 Desemba 2024Waziri Mkuu wa Italia, Giorgia Meloni amesema Urusi inatoa tishio kubwa la kiusalama kwa mataifa ya umoja wa ulaya kuliko inavyofikiriwa na kuonya kwamba Urusi inaweza kutumia njia ya uhamiaji haramu na masuala mengine kudhoofisha umoja huo.
Kiongozi huyo ameyasema hayo katika mkutano wa kujadili usalama na masuala ya uhamiaji katika nchi za Nordic na Mediterania uliofanyika hii leo nchini Finland. Mkutano huo uliwahusisha viongozi wa nchi za Italia, Sweden na Ugiriki pamoja na mkuu wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya.
Soma zaidi.Zelensky akutana na Meloni na kuomba silaha zaidi
Baadhi ya nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya kama Finland na Estonia zimeishutumu Urusi kwa kuruhusu wahamiaji haramu kutoka Mashariki ya Kati na kwingineko kuingia katika mataifa ya umoja huo bila ukaguzi, hatua hiyo inatajwa kuwa inadhoofisha usalama wa mataifa ya umoja wa ulaya.
Hata hivyo, Urusi imeyakanusha madai hayo kwamba inawaruhusu wahamiaji kuingia katika mataifa hayo kiholela.