1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

​​​​​​​Gladbach na Bayern Zapata ushindi muhimu

20 Oktoba 2016

Borussia Mönchengladbach ilipata pointi tatu muhimu katika ngome ya Celtic, wakati Bayern ikiifumania PSV mabao manne. Arsenal pia ilitamba wakati Manchester City ikiadhibiwa na Barcelona

https://p.dw.com/p/2RUWH
UEFA Champions League Celtic FC vs. Borussia Moenchengladbach
Picha: Getty Images/S. Welsh

Celtic 0–2 Borussia Mönchengladbach
(Stindl 57', Hahn 77')

Makosa mawili kutoka kwa beki Kolo Toure yaliizawadia Borussia Mönchengladbach ushindi usio na thamani dhidi ya Celtic na kuyaweka hai matumaini yao ya Champions League.

Gladbach ilikwenda Scotland bila ya wachezaji muhimu Thorgan Hazard, Raffael na Andreas Christensen, lakini ilitawala mchezo dhidi ya timu iliyoiteka Manchester City katika sare ya kusisimua ya 3-3 wiki mbili zilizopita. Lars Stindl aliweka langoni bao la kwanza la Gladbach kabla ya Andre Hahn kuyazika matumaini ya Celtic. Kichapo hicho sasa kimewaacha vijana hao wa Brendan Rodgers wakiwa mkiani mwa Kundi C, wakati Gladbach wangali na matumaini ya kutinga 16 ya mwisho baada ya ushindi huo wao wa kwanza wa ugenini barani Ulaya tangu mwaka wa 1977.

Bayern Munich 4–1 PSV Eindhoven

(Müller 13', Kimmich 21', Lewandowski 59', Robben 84' – Narsingh 41‘)

Bayern Munich iliweka kando matatizo yao ya kutopata ushindi katika mechi tatu mfululizo kwa kusajili ushindi mnono wa 4-1 dhidi ya PSV Eindhoven. Bayern ilichukua uongozi wa mapema wakati kona ya haraka yake Arjen Robben iliwapata PSV wakiwa usingizini, na Thomas Müller akaweka mpira wavuni.

Vijana hao wa Carlo Ancelotti waliongeza la pili katika dakika ya 20, baada ya chipukizi Joshua Kimmich kutia kimyani bao la kichwa ikiwa ni lake la saba msimu huu.

Masaibu ya PSV yaliongezeka baada ya Gaston Pereiro kukwepa mtego wa kuotea na kumfunga Manuel Neuer lakini bao hilo lilifutwa katika njia ya utata. Bahati ya PSV hata hivyo ilibadilika baada ya Luciano Narsingh kufunga bao safi sana, lakini Bayern iliweza kuongeza pengo la mabao kwa kufunga mawili kupitia kwa Robert Lewandowski na Arjen Robben.

Matokeo mengine ya Champions League:

Arsenal 6-0 Ludogorets

Barcelona 4–0 Man City

Dynamo Kiev 0-2 Benfica

Napoli 2-3 Besiktas

Paris Saint-Germain 3-0 Basel

Rostov 0-1 Atletico Madrid

Mwandishi: Bruce Amani/DW
Mhariri: Grace Kabogo