Guterres alaani vikali mauaji ya raia katika ukanda wa Gaza
21 Novemba 2023Guterres amewaambia waandishi wa habari kuwa, bila ya kuingia kwenye mjadala juu ya idadi kamili ya wahanga iliyochapishwa na mamlaka huko Gaza, kilicho wazi ni kwamba maelfu ya watoto wameuawa katika muda wa wiki chache.
Ameongeza kuwa, anashuhudia mauaji ya raia ambayo hayajawahi kutokea katika mzozo wowote tangu alipochukua nafasi ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.
Wakati hayo yakiarifiwa, wizara ya afya ya Gaza inayoendeshwa na Hamas imesema kuwa wagonjwa 100 wamehamishwa kutoka hospitali iliyojengwa kwa msaada wa serikali ya Indonesia.
Wagonjwa hao walihamishwa kwa usaidizi wa shirika la kimataifa la hilali nyekundu na msalaba mwekundu ICRC baada ya hospitali hiyo kushambuliwa na makombora ya Israel.
Msemaji wa wizara ya afya Ashraf al-Qudra ameliambia shirika la habari la AFP kuwa, wagonjwa wengine 100 pia watahamishwa usiku huu na kupelekwa katika kituo kingine cha matibabu katika mji wa kusini wa Khan Yunis.