1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Guterres hakwenda Congo ili Kabila afanye maamuzi 'muhimu'

Caro Robi
13 Julai 2018

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema amekubali kuahirisha ziara yake katika Jamhuri ya Kidemomkrasia ya Congo kumruhusu Rais Joseph Kabila kutangaza kile alichokitaja kuwa ni maamuzi muhimu.

https://p.dw.com/p/31NDF
Joseph Kabila Präsident der Demokratischen Republik Kongo
Picha: picture-alliance/dpa/M. Kappeler

Guterres alitarajiwa kuizuru Congo wiki hii wakati ambapo taifa hilo linajiandaa kufanya uchaguzi mkuu mwezi Desemba, uchaguzi ambao nchi za magharibi zinatumai zitafikisha ukingoni utawala wa Rais Kabila ambaye amekuwa madarakani tangu mwaka 2001.

Akizungumza na wanahabari katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York, Marekani, Katibu huyo mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema sababu alizopewa za kumtaka kuahirisha ziara yake Congo ni kuwa Rais Kabila hivi karibuni atatangaza maamuzi kadhaa muhimu.

Schweiz - UN-Generalsekretär in Genf
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio GuterresPicha: picture-alliance/Keystone/C. Zingaro

Hakufafanua zaidi ni maamuzi gani hasa lakini kuna matarajio kuwa Rais Kabila atatangaza rasmi kuwa hatagombea muhula mwingine madarakani. Guterres amesema Rais Kabila hataki kutoa taswira kuwa uamuzi wake umechukuliwa kutokana na shinikizo kutoka kwa jumuiya ya kimataifa.

Kabila ambaye amekuwa madarakani tangu mwaka 2001 hajaweka hadharani iwapo ataondoka madarakani licha ya shinikizo kutoka kwa Marekani, Ufaransa na Uingereza kumtaka atangaze wazi kuwa hatawania muhula mwingine.

Je, Kabila atang'atuka?

Muhula wake wa pili ulikamilika mwezi Desemba mwaka 2016. Makubaliano kati ya serikali yake, upinzani na asasi za kiraia yalimruhusu kusalia madarakani hadi Desemba mwaka jana, ambapo alitarajiwa kuitisha chaguzi na kuondoka madarakani.

Hata hivyo chaguzi hizo zimecheleshwa na kusababisha mzozo wa kisiasa katika taifa hilo lenye utajiri mkubwa wa madini na raslimali nyingine.

Guterres na balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Nikki Haley walikuwa wamepanga kuizuru Congo wiki hii lakini serikali ya nchi hiyo ilikataa kuwapokea, ikisema kwa sasa Rais Kabila anajishughulisha na maandalizii ya uchaguzi ujao.

Raymond Tshibanda N'tunga Mulongo
Mjumbe maalum wa Rais Kabila- Raymond TshibandaPicha: picture-alliance/dpa

Wagombea urais wana kati ya tarehe 25 mwezi huu hadi Agosti Mosi kuwasilisha kwa tume ya uchaguzi fomu za kutaka kuwania urais. Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limezidisha shinikizo kwa Congo kuelekea uchaguzi huo wa Desemba huku kukiwa na wasiwasi wa kuzuka ghasia.

Huku hayo yakijiri, Marekani imehusisha ongezeko la uwekezaji Congo na kuwepo chaguzi huru na za haki. Mjumbe maalumu wa Rais Kabila amesema Marekani imekuwa ikifungamanisha uwekezaji na uchaguzi, akiongeza kuwa hawahitaji shinikizo zaidi kuelewa msimamo wa Marekani.

Raymond Tshibanda amesema uchaguzi utafanyika kama ilivyopangwa na utakuwa huru na wa haki ili kuwathibitishia wakosoaji wa utawala wa Congo kuwa hawakuwa sahihi.

Marekani imesema chaguzi zitakazoendeshwa kwa njia iliyo sahihi,zitakuwa muhimu kwa kuamua mustakabali wa siku za usoni wa Congo na kanda nzima ya Afrika ya Kati.

Mwandishi: Caro Robi/Reuters/AFP

Mhariri:Josephat Charo