HANOI : Mkutano walenga Duru ya Doha na Korea Kaskazini
18 Novemba 2006Viongozi wa Asia na Pasifiki wamesema wako tayari kupunguza sana ruzuku za kilimo ili kufufuwa mazungumzo ya biashara duniani yaliokwenda kombo.
Katika taarifa iliotolewa leo hii katika siku ya kwanza ya mkutano wao wa siku mbili iliotawaliwa na kiwingu cha diplomasia juu ya suala la nuklea la Korea Kaskazini viongozi wa baraza hilo la Ushirikiano wa Kiuchumi wa Asia na Pasifiki wamesema wahusika wakuu katika kundi hilo wako tayari kujifunga katika kupunguza sana ruzuku ya kilimo katika nchi zao inayonekana kuvuruga mazungumzo ya biashara duniani yanayojulikana kama Duru ya Doha.
Taarifa hiyo ambayo haikutowa ufafanuzi zaidi imesema viongozi hao pia wameahidi kupunguza sana ushuru wa biashara za viwandani na kufunguwa njia mpya katika biashara ya huduma.
Juu ya suala la nuklea la Korea Kaskazini mshauri wa usalama wa Ikulu ya Marekani Stephen Hadley amesema viongozi hao wa APEC kwa kiasi kikubwa wamekubaliana juu ya taarifa ya kuongeza shinikizo kwa Korea Kaskaziani taarifa ambayo yumkini ikatolewa hapo kesho.
Hata hivyo Rais George W .Bush wa Marekani ameshindwa kumshawishi Rais mwenzake wa Korea Kusini Roh Moo- hyu kujiunga na mpango wa Marekani kuzidukiza na kuzikaguwa meli za Korea Kaskazini zinazoshukiwa kubeba zana kwa ajili ya kutengenezea silaha za nuklea.
Serikali ya Korea Kusini imesema inaunga mkono malengo ya mpango huo lakini inahofu kwamba utapelekea kuzuka kwa mapambano ya silaha.