Hatimaye ICC yatoa muelekeo wa siasa za Kenya
23 Januari 2012Huu ndio mwisho wa mitindo wa kutoandamwa kisheria wanasiasa na polisi wanaojihisi wanaweza kufanya wakitakacho.Ndio mwisho pia wa matumizi ya nguvu yaliyokithiri na mauwaji ya kikatili ambayo waliyoyafanya hawaandamwi. Watu wanaoandamwa na kuuliwa makanisani walikokimbilia, safisha safisha ya kikabila, mauwaji yaliyoandaliwa makusudi ya watoto, wakinamama na wakinababa.Yote hayo yatakoma hivi sasa.
Hadi wakati huu, wanasiasa nchini Kenya walihisi hawatoweza kuandamwa-kwasababu hata katika uchaguzi wa mwaka 1992 watu zaidi ya 700 waliuliwa na wahusika hawajawahi kufikishwa mahakamani.
Katika historia ya Kenya hadi wakati huu,hakuna mwanasiasa yeyote wa ngazi ya juu aliyelazimika kujieleza kutokana na visa vya uhalifu. Kuna usemi nchini Kenya: "yanini kumtafuta wakili, kama unaweza kumnunua hakimu ?". Nchi hiyo ya Afrika Mashariki ni miongoni mwa nchi zilizooza kwa rushwa ulimwenguni.
Baada ya matumizi ya nguvu yaliyokithiri yaliyofuatia uchaguzi wa mwaka 2007 na kuangamiza maisha ya zaidi ya watu 1300 na malaki wengine kutimuliwa toka maskani yao, vyombo vya sheria nchini Kenya vilidhihirika vimezidiwa na vimeshindwa kuunda mahakama yake yenyewe.Ndio maana mwendesha mashtaka mkuu wa korti ya kimataifa ya uhalifu, Luis Moreno-Ocampo, akasimamia kesi dhidi ya watuhumiwa.
Kesi hii ni onyo la The Hague kwa wanaovunja haki za binaadam kote ulimwenguni- hawatoweza tena kufanya maovu bila ya kuadhibitiwa.
Mandhari yote ya kisiasa nchini Kenya inaweza kubadilika kwa kuwa wawili kati wa washitakiwa ni wagombea katika uchaguzi wa rais wa mwezi Machi mwaka 2013.Uhuru Kenyatta ambae ni waziri wa fedha na pia makamo wa rais ambae pia ni mmojawapo wa matajiri wakubwa wa Kenya, na William Ruto aliyewahi kuwa waziri wa elimu na kilimo.
Wote wawili wanashikilia wana haki kwa mujibu wa katiba, kupigania wadhifa huo licha ya kufunguliwa mashtaka.
Wanaweza kuingia katika madaftari ya historia kama wagombea wa kiti cha rais waliofikishwa mahakamani mjini The Hague. Wadadisi wanaashiria kesi inaweza kudumu hadi miaka mitano.
Kwa mashirika yanayopigania masilahi ya jamii, siku ya leo ni siku ya kutia moyo inayowazidishia nguvu wazidi kutia kishindo mpaka wanasiasa hao wawili waachilie mbali matarajio yao.
Kwa wahanga hizo ni habari zinazowafanya wajipe matumaini;Ikiwa wanasiasa hawa wanne wa ngazi ya juu wameshitakiwa, basi hata Kenya korti ya taifa itafunguliwa kuwahukumu wengine kadhaa wanaohusika.
Uamuzi wa leo unafanya kuwa shida kwa yeyote yule mwengine kuandaa matumizi ya nguvu baada ya uchaguzi.Kilichosalia ni kutegemea kwamba ukurasa mpya umefunguliwa nchini Kenya na kwamba matumizi ya nguvu yanakoma na wenye kuvunja haki za binaadam daima watalazimika kujibu makosa yao tena bila ya kujali madaraka yake, wala kabila lake.
Mwandishi: Andrea Schmidt
Tafsiri: Oummilkheir Hamidou
Mhariri: Othman Miraji