Hatua ya kufungwa serikali yaendelea kuwatesa Wamarekani
14 Januari 2019Bunge la Marekani linaanza wiki nzima ya shughuli zake mjini Washington tangu chama cha Democrats kilipotwaa udhibiti wa bunge hilo.Hata hivyo kitakachowakabili wabunge ni maswali yale yale yanayoulizwa wakati wote.Je ni lini kufungwa kwa shughuli za serikali kutafikia kikomo?
Shughuli za serikali zimeendelea kufungwa nchini Marekani na rais Donald Trump hana dalili ya kutaka kuumaliza mgogoro huu. Mmoja wa maseneta kutoka chama cha Republican cha rais Trump anasema amempa rais huyo fikra juu ya uwezekano wa kuumaliza mgogoro huo ingawa anaamini huenda pia hatua yake ya kumshawishi Trump haitofanikiwa na ikaendelea kubakia kuwa matarajio. Seneta Lindsey Graham aliyezungumza na Trump kwa simu jana Jumapili amejaribu kumshawishi rais huyo kuzifungua tena shughuli za serikali kwa wiki kadhaa ili kutoa nafasi ya kuendeleza mazungumzo na chama cha Demokrats kuhusu mpaka anaotaka kuujenga kati ya Marekani na Mexico.Kufungwa shughuli za serikali kunawaathiri WaMarekani wengi miongoni mwao ni Aleshia Thompson mfanyakazi wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani.Kwa majonzi makubwa akiwa katika foleni ya kuchukua chakula cha msaada anasema.
''Kwanza kabisa kufungwa kwa serikali kumeniathiri kihisia. Sisi hakutaka iwe hivi ilivyo.Mimi ni mkongwe,nimeitumikia nchi hii ikiwa ni pamoja na kufanya kazi kwa zaidi ya miaka 35 katika wizara ya mambo ya nje. Ni nani aliyefikiria kwamba nitajikuta katika hali hii.kwahivyo nalazimika kujitafutia na kuitafutia familia yangu.''
Shughuli nyingi zimeingia kwenye msukosuko nchini humo ikiwemo shughuli za ukaguzi katika viwanja vya ndege. Kilichopo hivi sasa nchini Marekani ni kwamba ikiwa hakuna mwafaka utakaofikiwa kati ya Trump na chama cha Demokrats kufikia kipindi cha wiki tatu Graham anasema rais Trump atakuwa huru kuchukua hatua kubwa ya kutangaza hali ya hatari kitaifa. Lakini Seneta huyo wa jimbo la South Carolina anasema Trump bado anataka yafikiwe makubaliano juu ya kufadhili ujenzi wa ukuta kabla ya kukubaliana na fikra ya kufungua shughuli za serikali. Spika wa bunge Nancy Pelosi Mdemocrat anasisitiza kwamba Trump anapaswa kwanza kuifungua tena serikali. Chama cha Democrats kinapinga hatua ya kutangazwa hali ya hatari lakini huenda chama hicho hakina mamlaka ya nguvu za kuzuia hatua hiyo kuchukuliwa na Trump. Mgogoro huu umeendelea kwa wiki kadhaa sasa na shughuli za serikali zimefungwa leo ikiwa ni siku ya 24 na hakuna ishara ya wazi inayoonesha kwamba utamalizika haraka.
Mwandishi:Saumu Mwasimba
Mhariri:Iddy SseSsanga