1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Heynckes asema Bayern wana hamu kubwa

29 Desemba 2012

Kukaa miaka miwili bila taji kumemfanya kila mchezaji katika klabu ya Bayern Munich kutia bidii katika juhudi za kushinda tena mataji mwishoni mwa msimu huu. Haya ni kwa mujibu wa mkufunzi Bayern Munich Jupp Heynckes

https://p.dw.com/p/17B7w
Munich's scorer Ivica Olic (L) and coach Jupp Heynckes celebrate the 1-0 goal during the Champions League quarter final second leg soccer match between FC Bayern Munich and Olympique Marseille at the Allianz Arena in Munich, Germany, 03 April 2012. Photo: Marc Müller dpa/lby
Champions League Viertelfinale FC Bayern München Olympique de MarseillePicha: picture-alliance/dpa

Heynckes anasema katika mahojiano yaliyochapishwa katika tovuti ya klabu hiyo kwamba viongozi hao wa ligi kwa sasa wameonyesha matokeo ya kuridhisha kufikia sasa, lakini kwamba tathmini ya mwisho inaweza tu kufanywa mwishoni mwa msimu. Munich hawajashinda taji mwaka wa 2011 na 2012, wakamaliza wa pili nyuma ya Borussia Dortmund katika Bundesliga na Kombe la Shirikisho DFB Pokal, na kushindwa katika fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, Champions League dhidi ya Chelsea kupitia mikwaju ya penalti katika uwanja wao wa nyumbani Allianz Arena. Na sasa klabu hiyo yenye Tayari inaongoza kileleni na tofauti ya pointi tisa, itachuana na Dortmund katika robo fainali ya DFB Pokal, na kukutana na Arsenal katika awamu ya mwondowano ya Champions League.

Holtby kuondoka Schalke04

Kiungo wa Ujerumani Lewis Holtby, anayedaiwa kumulikwa na vilabu vya Ligi ya soka ya England, ataondoka klabu ya Schalke04 kwa uhamisho huru baada ya kukamilika msimu huu. Taarifa ya Schalke imesema Holtby mwenye umri wa miaka 22 amewaambia maafisa wa klabu hiyo ya Bundesliga kwamba amekataa kusaini mkataba mpya baada ya mwaka wa 2013. Vilabu vya England, Tottenham, Arsenal na Liverpool vinadaiwa kuwa na nia ya kumsajili chipukizi huyo.

Kuingo wa Schalke Lewis Holtby kuondoka mwishoni mwa msimu
Kuingo wa Schalke Lewis Holtby kuondoka mwishoni mwa msimuPicha: dapd

Kwingineko, mkufunzi mpya wa klabu ya Wolfsburg Dieter Hecking, ameelezea matumaini ya kuwa na mwanzo bora baada ya mapumziko ya msimu wa baridi, ili kumaliza kipindi kigumu kigumu katika klabu hiyo. Hecking amezinduliwa rasmi kama kocha wa tatu wa klabu hiyo msimu huu kufuatia kuondoka kwa Fekix Magath aliyeondoka mwezi Oktoba, na kocha wa muda Lorenz-Guenther Koestner. Hecking amejiunga na Wolfsburg kwa mkataba wa hadi mwaka wa 2016 kutoka klabu ya Nuremberg. Wolfsburg wako katika nafasi ya 15 ya Bundesliga na pointi 19, pointi saba kutoka eneo la kushushwa daraja.

Sheria kuhusu usajili wa wachezaji

Na katika suala jingine ambalo wengi tunasubiri kuona ni, vilabu kuanza kuwasajili wachezaji wapya katika kipindi cha usajili Januari, lakini sasa huku kukiwa na sheria mpya za kifedha kutoka wka shirikisho la soka Ulaya UEFA, vilabu vikuu vya ligi hiyo vitafanya usajili kwa tahadhari kubwa. Lakini baadhi ya biashara inayofanywa katika kipindi hiki haijakuwa ya kufana huku wachezaji wanaonunuliwa wakishindwa kutamba katika vilabu vipya. Kwa mfano Liverpool waliiuzia Chelsea mshambuliaji Fernando Torres kwa kitita kikubwa zaidi Uingereza pauni milioni 50, na kutumia pauni milioni 35, kwa Andy Caroll aliyeshindwa kung'aa vile vile.

Mshambuliaji wa Dortmund Robert Lewandowski anamulikwa na Manchester United
Mshambuliaji wa Dortmund Robert Lewandowski anamulikwa na Manchester UnitedPicha: AFP/Getty Images

Liverpool pia walipata huduma za mshambuliaji Luis Suarez ambaye amekuwa mmoja wa washambuliaji wakali sana wa katika ligi, lakini mkufunzi wa United Sir Alex Ferguson anasema Januari ni wakati mbaya wa kufanya bishara. Sheria hiyo ya UEFA inalenga kuvizuia vilabu dhidi ya kutumia kiasi kikubwa cha fedha kuliko uwezo wao na tangazo la wiki iliyopita kwamba Malaga inayokumbwa madeni itapigwa marufuku dhidi ya kushiriki vinyang'anyiro vya Ulaya kwa mwaka mmoja linadokeza kwamba mpango huo huenda ukawa na makali zaidi kuliko jinsi wakosoaji wake wanavyodai.

Vilanova kurejea katikati ya Januari

Kule Uhispania, rais wa klabu ya Barcelona Sandro Rosell amesema kocha Tito Vilanova ambaye anaugua maradhi ya saratani atarudi kazini katikati ya mwezi Januari. Vilanova amefanyiwa upasuaji tarehe 20 Desemba, siku moja baada ya klabu hiyo kutangaza kwamba hali ya kocha huyo mwenye umri wa miaka 44 haikuwa nzuri. Alitibiwa kwa mara ya wkanza mwaka wa 2011. Barcelona waliweka rekodi ya kuwa na mwanzo mzuri katika msimu wao wa kwanza chini ya Vilanova, ambaye alichukua viatu vya Pep Guardiola, kwa kupoteza pointi mbili pekee katika mechi 17 na kuwa na uongozi wa tofauti ya pointi tisa kileleni. Naibu wake Jordi Roura amechukua nafasi yake. Mchuano unaokuja wa Barca katika La Liga utakuwa nyumbani dhidi ya watani wao wa mji Espanyol mnamo Janauri 6.

Tito Vilanova anaendelea kupata nafu baada ya kufanyiwa upasuaji
Tito Vilanova anaendelea kupata nafu baada ya kufanyiwa upasuajiPicha: picture-alliance/dpa

Nadal ajiondoa Australian open

Katika tennis, nyota wa Uhispania Rafael Nadal amechelewesha kurejea kwake hadi mwishoni mwa Februari, akisema maradhi ya tumbo yamemfanya kukosa kinyang'anyiro cha Australian Open na mashindano mengine. Mchezaji huyo aliyekuwa nambaro moja ulimwenguni, hajaingia uwanjani tangu alipoondoka uwanjani katika raundi ya pili ya kinyang'anyiro cha Wimbeledon mnamo Juni 28. Amekuwa mkekani kutokana na jeraha la kifundo ambalo lilihitaji upasuaji, na alipanga kurudi uwanjani wiki hii katika maonyesho ya Abu Dhabi, lakini akawacha kutokana na maradhi ya tumbo.

Mwandishi: Bruce Amani/reuters/DPA/AFP/AP

Mhariri: Mohammed Dahman