Hiddink: Chelsea inaweza kucheza Champions League
5 Januari 2016Hayo ni kwa mujibu wa kocha wa mpito Guus Hiddink. Chelsea imeipiga mwereka Crystal Palace kwa mabao 3-0 jana, na kusajili ushindi wake wa sita msimu huu na ushindi wa kwanza chini ya kocha Hiddink tangu alipotwaa hatamu za uongozi wa timu hiyo kutoka kwa Jose Mourinho mwezi uliopita.
Ushindi huo umeisogeza Chelsea hadi nafasi ya 14 na pointi 13 nyuma ya timu inayokamata nafasi ya nne Tottenham Hot Spurs , na Hiddink amekataa kufuta uwezekano wa timu yake kufikia nafasi ya nne , licha ya kukiri kwamba itakuwa kazi pevu.
Kocha Claudio Ranieri hasumbuliwi na ukame wa magoli uliokumba timu yake ya Leicester na anasema ni suala la muda tu kabla ya mbweha hao kuanza kuzitafuna tena nyavu kama kawaida yao.
Leicester walikuwa kileleni mwa msimamo wa ligi wakati wa sikukuu ya Krismass, lakini waliporomoka hadi nafasi ya pili nyuma ya Arsenal baada ya sare ya bila kufungana na Bournemouth siku ya Jumamosi.
Mwandishi: Sekione Kitojo / dpae / afpe / rtre
Mhariri: Mohammed Khelef