Hoffenheim kuikabili Man. City Champions
1 Oktoba 2018Hoffenheim itakutanna na Man. city katika uwanja wake wa nyumbani, Rhein Neckar Arena.
Kocha wa Hoffenheim Julian Nagelsmann ambaye ndiye mwenye umri mdogo zaidi miongoni mwa makocha wa vilabu vinavyoshiriki michuano hiyo na hata Bundesliga, akiwa na umri wa miaka 31 ndiye kocha wa kwanza wa umri kama huo kufanikiwa kufikia hatua hii ya michuano ya Champions. Hata hivyo amekiri ugumu anauona katika kundi F alilopangwa.
Hoffenheim alianza michuano hiyo kwa ushindi wa kishindo, ikiwa ugenini dhidi ya Shakhtar Donetsk. Hoffenheim, iko nafasi ya 11 katika msimamo wa ligi ya Bundesliga, baada ya kichapo cha Jumamosi iliyopita ilichokipata toka kwa RB Leipzig, klabu ambayo Nagelsmann ataanza kuifundisha, ifikapo majira yajayo ya joto.
Wiki hii pia, mabingwa watetezi wa Bundesliga, Bayern Munich walioko kundi E wataialika klabu ya Ajax, ya nchini Uholanzi katika uwanja wake wa Allianz Arena, mjini Munich, huku Borussia Dortmund iliyoko kundi A ambayo bado itakuwa na furaha ya ushindi mnono wa mabao 4-2 dhidi ya Bayer Leverkusen wa Jumamosi iliyopita yenyewe ikiwa mwenyeji wa Monaco, katika mechi itkayopigwa kwenye uwanja wake wa nyumbani Signal Iduna Park.
Lokomotiv Moskva ya Urusi, itaikaribisha Schalke 04, ambayo hivi sasa inashikilia nafasi ya pili kutoka mwisho katika msimamo wa Bundesliga, baada ya ushindi mwembamba wa Jumamosi ikiwa nyumbani dhidi ya Mainz 05 wa bao 1-0.
Mwandishi: Lilian Mtono/DPAE
Mhariri:Josephat Charo