El Nino kambi za wakimbizi Tanzania
23 Novemba 2015Tahadhari hiyo imetolewa na mashirika ya misaada siku ya Jumatatu kufuatia kuongezeka kwa mgogoro wa kisiasa na hali mbaya ya usalama nchini Burundi .
Magonjwa ya malaria na kuhara yanaelezwa kuenea kwa kasi katika kambi ya Nyarugusu, kambi ya tatu kwa ukubwa, tangu kuanza kwa msimu wa mvua unaoambatana na madhara yanayotokana na El Nino, na kufanya mashirika hayo kuwa na upungufu wa fedha za kuendeshea kambi hizo katika Afrika ya Mashariki.
Taarifa ya mashirika ya misaada yakiwemo mashirika ya Oxfam, Save the Children na HelpAge ilisema “Mamia ya wakimbizi wanawasili kila siku” na kuongeza kuwa wengi wa watu waishio katika kambi hizo bado wanasongamana na kwamba kutokana na msongamano huo, kuna hatari kubwa ya kambi hiyo kukumbwa na magojwa yanayosababishwa na vimelea vinavyotokana na mafuriko na magonjwa mengine ya kuambukizwa.
Kipindupindu huenda kikazuka tena
Mashirika hayo pia yameonesha wasiwasi wake wa kwamba huenda kukaripuka tena ugonjwa wa kipindupindu, ugonjwa ambao uliua wakimbizi 33 wa kutoka Burundi mwezi May. Wasiwasi wa mashirika hayo unafuatia na ukweli kwamba baada ya mvua kubwa kunyesha, vyoo vingi hufurika.
Kuanzia mwezi wa April kumekuwa na ongezeko kubwa la watu wanaowasili katika kambi hiyo na nyingine zilizoko Tanzania. Kambi ya Nyarugusu inawakimbizi 180,000 kutoka katika nchi za Burundi na Kongo. Ongezeko hilo la wakimbizi linafuatia uamuzi tata wa Rais wan chi hiyo Pierre wa kugombea tena nafasi hiyo kwa awamu ya tatu.
Watu 240 waliuawa na na wengine zaidi ya 200,000 wamekimbilia katika nchi za jirani kufuati vurugu zilizoibuka katika nchi hiyo.
Nkurunzinza alishinda uchaguzi wa July mwaka huu, na tangu baada ya ya ushindi wake kumekuwa na mapigano kati ya waandamanaji na vikosi vya usalamakatika mji mkuu wa nchi hiyo Bujumbura, na mfululizo wa mauaji ya walengwa.
Mgogoro wa Burundi chanzo cha kuongezeka wakimbizi
Taarifa hiyo imesema kuongezeka kwa migogoro ya kisiasa ndani ya Burundi kumeongeza hofu na misafara mipya wa wakimbizi katika
nchi jirani, suala ambalo linaweza kushinikiza kuongezeka zaidi kwa idadi ya sasa ya wakimbizi waliopo katika kambi magharibi mwa Tanzania.
Waburundi wanaishi katika mazingira magumu katika kambi hizo kwakuwa wanaishi katika makazi ya dharula, Huku wenzao kutoka Kongo wakiwa katika mazingira bora zaidi kwasababu wamekuwa wakiishi katika kambi hizo kwa muda mrefu zaidi.
Ilikupunguza msongamano katika kambi ya Nyarugusu, zaidi wa wakimbizi 50,000 walihamishiwa katika kambi ya pili ya Nduta, kilomita 100 kaskazini mwa Nyarugusu na kwamba kambi nyingine ya tatu inategemewa kuanzishwa.
Kwa mujibu wa umoja wa mataifa, mafuriko ya El Nino yanatazamiwa kuwa makubwa kuwahi kuripotiwa ambayo tayari yamesababisha mafuriko katika nchi za Afrika ya mashariki hasa katika nchi za Kenya na Somalia na hivyo kuweka maisha ya watu milioni mbili katika hatari ya kutokuwa na makazi na kukumbwa na magonjwa.
Mwandishi: Mwazarau Mathola/ RTRE
Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman