Hofu za siasa zaikosesha DRC bashasha za Krismasi
25 Desemba 2018Ni siku ya Krismasi, lakini katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo hali sio ya shamrashamra na sherehe kama inavyotarajiwa katika siku ya Krismasi. Raia wa nchi hiyo wana wasiwasi iwapo uchaguzi ulioahirishwa utafanyika Jumapili tarehe 30 Desemba wiki hii kama ilivyoahidiwa.
Wiki iliyopita, upinzani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ulikubali uamuzi wa tume inayosimamia uchaguzi CENI wa kusogeza mbele kwa siku saba uchaguzi uliopaswa kufanyika tarehe 23 Desemba. Upinzani umetishia kufanya maandamano makubwa ikiwa uchaguzi utaahirishwa tena.
Kwenye mahubiri ya Krismasi katika kanisa la Notre Dame mjini Kinshasa, askofu Fridolin Ambongo amesema amani ya kweli inategemea ikiwa utawala wa nchi hiyo utatimiza ahadi zake za kisiasa, na amesisitiza kwa kusema ili kuwe na amani nchini Kongo, ni lazima uchaguzi ufanyike tarehe hiyo iliyopangwa Desemba 30 mwaka 2018. Askofu Ambongo ameendelea kusema:
"Ili amani ya kweli iwepo, matokeo yatakayochapishwa, yanahitaji yaonyeshe matakwa kamili ya watu kama jinsi walivyopiga kura. Matokeo ambayo hayataonesha yale watu wanayoyataka yatamaanisha kuingamiza amani katika nchi yetu."
Katika misa ya mkesha wa Krismasi baadhi ya waumini wa kanisa Katoliki katika mji wa Kinshasa walielezea jinsi machafuko na hali isiyotabirika kisiasa inavyowatia wasiwasi. Mmoja wao ni Yannick Tshimanga ambaye ndugu yake aliuawa kwa kupigwa risasi katika eneo la kanisa kufuatia machafuko ya siasa mwezi Februari:
"Tunasherehekea siku ya kuzaliwa kwa Yesu lakini watu wana msongo wa mawazo. Kuna watoto ambao wazazi wao wameuawa chini ya utawala wa sasa ambao wanasherehekea Krismasi bila wazazi wao. Haya ndiyo mazingira tunayosherehekea Krismasi”
Ikiwa uchaguzi wa rais katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ambao sasa umeahirishwa mara tatu utafanyika Jumapili tarehe 30, basi utafikisha mwisho utawala wa rais Joseph Kabila ambaye ameiongoza nchi hiyo kwa miaka 18.
Mwandishi: John Juma/RTRE
Mhariri: Zainab Aziz