1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bemba aachwa nje ya orodha ya uchaguzi Congo

25 Agosti 2018

Tume ya uchaguzi ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo imemuacha nje kiongozi wa upinzani Jean-Pierre Bemba kutoka kwenye orodha iliyochapishwa Ijumaa, ya wagombea walioidhinishwa kushiriki uchaguzi wa urais wa Desemba.

https://p.dw.com/p/33jTs
Niederlande Kongo Jean-Pierre Bemba Gombo wegen Kriegsverbrechen in Den Haag verurteilt
Picha: picture-alliance/dpa/EPA/M. Kooren

Bemba ni mbabe wa zamani wa kivita ambaye alirudi Congo kuwasilisha ugombea wake wa urais baada ya mwongo mmoja akiwa katika jela ya The Hague alipokuwa amefungwa kwa makosa ya uhalifu wa kivita na alikuwa anaonekana kama mmoja wa waliokuwa mstari wa mbele kuichukua nafasi ya Joseph Kabila.

Tume hiyo imesema Bemba ameachwa nje kwasababu ya kifungo cha kando alichopewa na mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita ICC kwa kosa la kuharibu ushahidi. Bemba aliachiwa huru na mahakama ya ICC baada ya kukata rufaa dhidi ya madai ya mauaji, ubakaji na utekaji nyara, mambo yaliyofanywa na wapiganaji aliowatuma katika Jamhuri ya Afrika Kati mwaka 2002 ila kifungo chake cha kuharibu ushahidi bado kipo.

Bemba alikuwa katika nafasi ya tatu kwenye kura ya maoni mwezi Julai

Mawaziri wakuu wa zamani Adolphe Muzito, Antoine Gizenga na Samy Badibanga ni miongoni mwa wagombea sita walioachwa nje ya orodha ya tume hiyo. Vyama vya upinzani vimelaani uamuzi wa tume hiyo ya uchaguzi ambao unaweza kukatiwa rufaa kabla orodha ya mwisho haijachapishwa mwezi Septemba.

Kongo Ankunft Oppositionsführer Jean-Pierre Bemba
Wafuasi wa Bemba wakimkaribisha KinshasaPicha: Reuters/K. Katombe

Katika taarifa ya pamoja vyama hivyo vimesema "kwa mara nyingine uongozi wa sasa unaonyesha juhudi zake za kukandamiza mchakato wa uchaguzi."

Mwezi uliopita Bemba alikuwa katika nafasi ya tatu kwenye kura ya maoni ya nadra iliyoonyesha matarajio ya matokeo ya uchaguzi huo ambapo alipata uungwaji mkono wa asilimia 17.

Ana umaarufu magharibi mwa Congo ikiwemo katika Mji Mkuu Kinshasa na kutojumuishwa kwake kunaweza kuwapelekea wafuasi wake wazue machafuko. Baada ya Bemba kushindwa na Kabila katika uchaguzi wa mwaka 2006 kulizuka machafuko mitaani kati ya wanamgambo watiifu kwa Bemba na kikosi cha serikali.

Kabila ana lengo la kuhusika na siasa za Congo katika miaka ijayo

Mapema mwezi Agosti Kabila aliitii katiba ya nchi hiyo inayotaka rais ahudumu kwa mihula miwili pekee, kwa kutowasilisha jina lake kuwa miongoni mwa wagombea katika uchaguzi huo wa Desemba 23.

DRC Präsident Joseph Kabila
Rais Joseph Kabila wa CongoPicha: Reuters/K.Katombe

Badala yake alimchagua waziri wa zamani wa mambo ya ndani, ambaye amewekewa vikwazo na Umoja wa Ulaya awanie urais.

Hatua yake ya kumchagua mtu ambaye ni muaminifu kwake ilileta picha kwamba rais huyo ambaye aliingia uongozini baada ya kuuwawa kwa babake mwaka 2001, ana lengo la kuhusika kwa karibu na siasa za taifa hilo.

Kabila atakubaliwa kuwania tena urais mwaka 2023.

Mwandishi: Jacob Safari/Reuters/AFPE

Mhariri: Bruce Amani